Mbaroni kwa vipande 14 vya meno ya tembo

POLISI mkoani Kigoma kwa kushirikiana na askari wa uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Gombe mkoani Kigoma, wamemtia mbaroni mtu mmoja anayeaminika kuwa mtumishi wa afya katika Halmashauri ya Wilaya Uyui mkoani Tabora akiwa na vipande 14 vya meno ya tembo. 

Kamanda wa Polisi Mkoa Kigoma, Filemon Makungu akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mjini Kigoma alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa mwishoni mwa mwezi uliopita katika Kijiji cha Kidyama, Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.

Kamanda Makungu ambaye alikataa kutaja jina la mtuhumiwa aliyekamatwa kwa madai isije kuharibu upelelezi, alisema kuwa meno hayo yenye uzito wa kilo 20.4 yana tahamani ya shilingi milioni 26.4.

 Mkuu wa kikosi cha  misitu na Uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Gombe,  Yustin Njamasi alisema kuwa kukamatwa kwa vipande hivyo 14 kunatokana na mchango mkubwa wa taarifa za wananchi, ambao umefanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo.

 Alisema kuwa mtuhumiwa huyo si mkazi wala mtumishi wa mkoa Kigoma na hiyo inathibitisha kwamba huo ni mtandao wa watu, hivyo bado uchunguzi unafanyika kubaini mtandao huo, ili kuchukua hatua zaidi kwa wanaohusika na mtandao huo.

 Mkuu huyo wa kikosi alisema kuwa katika kupitia na kukagua meno hayo wamegundua kuwa yamekatwa katwa kutoka kwenye jumla ya tembo watatu, ambao wameuawa hivyo upelelezi kuhusiana na tukio hilo unaendelea.

Sambamba na tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa Kigoma amezungumzia kukamatwa kwa wahamiaji haramu 78 walioingia, kuishi na kufanya kazi mkoani humo, wakiwa hawana nyaraka zozote zinazowaruhusu kufanya hivyo na kwamba idadi kubwa ya wahamiaji hao ni raia kutoka nchini Burundi.

Habari Zifananazo

Back to top button