Mbeki ahimiza umoja Afrika

RAIS mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki amewahimiza Waafrika kudumisha umoja na kuwaenzi waasisi wa harakati za ukombozi.

Amesema hayo wakati katika ziara mkoani Morogoro kutembelea eneo la kihistoria ya Mazimbu (Solomon Mahlangu) ambalo ni kitovu cha wapigania uhuru wa African National Congress (ANC) waliokuwa uhamishoni wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi.

Alisema Tanzania chini ya Uongozi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ilitoa mchango mkubwa wa mapambano ya ukombozi wa nchi nyingi barani Afrika, ikiwemo Afrika Kusini.

Mbeki alisifu Uongozi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kuweza kulitunza eneo la makaburi ya wapiganaji wa ANC na kwamba eneo hilo litabaki kuwa ni kitovu cha kumbukumbu ya watu wa Afrika Kusini na wengineo.

“Watu wetu wa Afrika Kusini, jamaa na ndugu za marehemu waliozikwa hapa Mazimbu wanapokuja kutembelea eneo hili watakumbuka nini kilifanyika Mazimbu, nini kilifanyika Morogoro kwa namna ambavyo Waafrika wenzao walivyoweza kujitoa kupigania uhuru wa nchi yao, ni eneo lenye kumbukumbu muhimu sana,” alisema
Mbeki.

Ziara ya Mbeki ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Afrika, yanayoadhimishwa kila mwaka Mei 25, ikiwa ni kumbukumbu ya kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika na kuhamasisha mshikamano, maendeleo na utambulisho wa bara la Afrika.

Rais Mbeki yuko nchini kwa mwaliko wa Taasisi ya Thabo Mbeki kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Tanzania na pamoja wameandaa maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Afrika.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima kwa niaba ya Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na wananchi wa mkoa huo alimshukuru, Mbeki kwa kutembelea eneo hilo la kihistoria kwa ukombozi wa Afrika Kusini.

Alisema waliozikwa eneo la Mazimbu ni watu wa kutoka nje ya nchi lakini wananchi wa Morogoro waliridhia wazikwe hapo kutokana na harakati za mapambano ya kudai uhuru wa nchi yao ya Afrika Kusini.

Naibu Makamu Mkuu wa SUA (Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu), Profesa Maulid Mwatawala kwa niaba ya Uongozi wa SUA alisema chuo hicho kitaendelea kusimamia maeneo yaliyotumika wakati wa harakati za ukombozi wa Afrika Kusini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button