Mbogwe wafanya kweli kudhibiti udumavu

HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita imefanikiwa kutoa matone ya Vitamin A kwa watoto 55,928 kati ya watoto 56,442 sawa na asilimia 99 ya mafanikio ikiwa ni sehemu ya kudhibiti udumavu.

Ofisa Lishe Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe, Norah Massawe ametoa taarifa hiyo kwa viongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023 walipotembelea zahanati ya kijiji na Kata ya Ilolanguru.

Amesema takwimu hizo ni kuanzia Julai 2022 hadi Juni, 2023 ambapo watoto waliolengwa ni walio katika umri wa miezi sita mpaka 59 ili kutokomeza udumavu, uzito pungufu na ukondefu kwa watoto.

Norah ameongeza, pia kina mama na walezi 93,151 wamepatiwa elimu ya unyonyeshaji, uandaaji wa chakula cha nyongeza pamoja na ulishaji kwa watoto wadogo walio na umri kati ya miezi sita.

Amesema wameweka msisitizo kwa kina mama kuanza kunyonyesha mapema ndani ya saa moja la kwanza baada ya kujifungua na kunyonyesha maziwa ya mama pekee ndani ya kipindi cha miezi sita.

Amesema takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2018 zinaonesha Mkoa wa Geita unakabiliwa na udumavu kwa asilimia 38.6, uzito pungufu asilimia 16.2 na ukondefu asilimia 2.8.

Ameeleza, kwa kuliona hilo halmashauri imeimarisha utolewaji wa vidonge vya madini chuma ili kuzuia kuzaliwa watoto wenye vichwa vikubwa na vidogo, mgongo wazi, mdomo sungura, na uzito pungufu.

Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2023, Abdallah Shaib Kaim amewaomba wazazi na walezi kuzingatia taratibu za utoaji chakula bora kwa kuzingatia makundi yote ya chakula kwa watoto.

Amesema hali hiyo itasaidia kutekelezwa kwa vitendo kampeni ya kukabiliana na tatizo la udumavu, uzito pungufu na ukondefu kwa watoto na kuongeza idadi ya watoto wenye afya bora na imara kwa watoto.

Habari Zifananazo

3 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button