Mbowe ataja faida maridhiano na serikali

Freeman Mbowe

DAR ES SALAAM; MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amezitaja faida za maridhiano kati ya chama chake na serikali pamoja na kutangaza nia ya kutetea nafasi ya uenyekiti katika chama hicho.

Sasa atachuana na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu ambaye alishachukua fomu ya kuwania uenyekiti wa chama hicho.

Awali alisema ili nchi ipate maendeleo ni lazima kukaa chini na kuzungumza ili kupata ajenda moja.

Advertisement

Mbowe alisema hayo wakati wa mkutano na wahariri na waandishi wa habari uliofanyika nyumbani kwake Mikocheni, Dar es Salaam jana.

“Dhana ya kuwa na maridhiano yaliyofanyika kati yangu na Rais Samia Suluhu Hassan hayakuwa na faida yoyote kwa chama ni potofu, kwani moja ya faida iliyopatikana ni viongozi wote waliokuwa uhamishoni kurejea nchini na kufutiwa kesi zilizokuwa zikiwakabili ikiwemo mimi na Joseph Mbilinyi,” alisema Mbowe.

Aliongeza: “Kupitia maridhiano tumefaidika pakubwa kwani wafuasi wetu wameachiwa huru na kufutiwa kesi 460 zilizokuwa zikiwakabili huku zikibaki kesi mbili za Njombe na Kibaha”.

Alisema faida nyingine ni kurejeshwa kwa mikutano ya hadhara ya kisiasa pamoja na maandamano yaliyokuwa yamezuiliwa kwa miaka saba, hivyo bila maridhiano yote yasingerejeshwa.

Mbowe aliongeza kuwa kurejeshwa kwa ruzuku za chama zaidi ya Sh bilioni mbili ambazo hazikutolewa na serikali kwa kipindi kirefu lakini kwa kipindi cha maridhiano fedha hizo zimeletwa na kutumika kununua Jengo la Makao Makuu ya chama hicho eneo la Mikocheni.

Mbowe alisema madai ya kuahidiwa kinachoitwa serikali ya nusu mkate ni madai ya uongo.

Alisema kuwa endapo wasingeingia kwenye maridhiano, wasingeshiriki kwenye uchaguzi wowote.

“Jambo hili halijawahi kuwa ajenda ya Chadema kwenye vikao vya Kamati Kuu, kwenye vikao vya Kamati ya Maridhiano, wala kwenye hoja 11 tulizopeleka kwa Rais (Samia) na kwenye kamati ya maridhiano hatujawahi kulijadili jambo hili na mahali kokote naomba nieleweke hivyo,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema maridhiano yamelenga kujenga umoja unaoleta maendeleo na si vingine.

Maridhiano kati ya Mbowe na Serikali yanatokana na falsafa ya 4R ya Rais Samia ambayo ni Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko na Kujenga Upya.

Aidha, Mwenyekiti huyo alisema hawezi kuondoka katika chama hicho wakati kikiwa kwenye mnyukano bali atagombea ili kuitetea nafasi yake, hivyo kura zitaamua.

“Mimi bado nipo sana kwenye chama na tushirikiane katika kukiendeleza chama chetu na natangaza rasmi kuwa baada ya kutoka hapa nitaenda makao makuu kwa ajili ya kuchukua fomu ya kugombea uenyekiti,” alisema.

Kadhalika, alieleza kuwa yupo tayari kufanya kazi na mtu yeyote, ikiwemo Lissu endapo atachaguliwa mwenyekiti badala yake, kwamba chama hicho kinahitaji kujengwa kwa ushirikiano na kinamuhitaji kila mtu.

Akijibu tuhuma za kula fedha za chama, Mbowe alisema hakuanza kukifadhili chama hicho leo na historia nzima ipo kwa waasisi wachache ambao wapo.

“Kama bado wapo hao viongozi wanajua ni kwa kiasi gani nimekiunga mkono chama na mimi ni mfanyabiashara wa ndani na nje ya nchi, namiliki mali ndani ya nchi na nje ya nchi, mimi sio mbangaizaji,” alisema.

Akizungumzia kuhusu kuwarejesha wabunge 19 wa chama hicho walioondolewa uanachama, alisema yeye hana mamlaka ya kuwarejesha bali wao ndio wanaweza kuomba msamaha kwa chama ili kiweze kuwarudisha na pia watarejea kwa mujibu wa taratibu za katiba ya chama hicho.