Mbunge ahoji urasimishaji vijana wa ujuzi nje ya mfumo

SERIKALI imeweka mkakati kupitia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano wa kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo kwa vijana 100,000 ifikapo 2025/2026.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Patrobas Katambi alitoa kauli hiyo bungeni Dodoma jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Singida Mjini, Mussa Sima (CCM) aliyetaka kujua kuna mkakati gani wa kurasimisha vijana waliopata ujuzi nje ya mfumo rasmi.

Aidha, katika utekelezaji wake hadi kufikia Juni 2022 kupitia Programu ya Taifa ya kukuza ujuzi, vijana wapatao 22,296 (wa kike 3,349 na kiume 18,947) kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara wamerasimishwa ujuzi wao.

Katambi alisema kuna fani kumi zinazohusika katika urasimishaji ambazo ni uashi, useremala, ufundi magari, upishi na uhudumu wa hoteli, baa na migahawa, ufundi bomba, unyooshaji bodi za magari, umeme wa majumbani, ushonaji nguo na uchomeleaji vyuma.

Aidha, kutokana na manufaa wanayoyapata vijana, katika mwaka wa fedha 2022/2023, jumla ya vijana 18,445 (wa kiume 13,873 na wa kike 4,572) wamejitokeza na kujaza fomu kwa ajili ya kurasimishwa ujuzi wao kupitia programu hii ambapo taratibu zinakamilishwa ili waweze kupatiwa fursa hiyo.

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Husna Sekoboko (CCM) aliyetaka kujua serikali ina mkakati gani wa kuwapa vyeti vya kutambulika vijana wote ambao wanakuwa wamerasimisha ufundi wao ili kupata ajira katika taasisi mbalimbali, Katambi alijibu kuwa vijana wote wanaokuwa wamerasimisha ufundi wao wanatakiwa kupewa vyeti ili kuhakikisha wanatambulika.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button