MBUNGE wa Jimbo la Mlimba lililopo mkoani Morogoro, Godwin Kunambi ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha za kujenga barabara ya kiwango cha lami kutoka Ifakara hadi Mbingu na baadaye kuikamilisha hadi Chita.
Ujenzi wa barabara hiyo utafanywa na Mkandarasi wa Kampuni ya M/s Henan Highway Engineering Group Co. Ltd ya kichina ambayo imepewa zabuni ya kujenga barabara ya Ifakara-Kihansi yenye urefu wa kilometa 124 sehemu ya kwanza Ifakara-Mbingu ya kilometa 62.5 kwa kiwango cha lami.
Kunambi ametoa shukrani hizo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mbingu, kata ya Igima ambao ulikuwa ni maalumu kwa ujio wa Waziri Ujenzi , Innocent Bashungwa alipokwenda kukagua mitambo ya mkandarasi .
Mbunge huyo amesema kilio chao kikubwa cha wananachi ni kupata barabara ya lami ambapo kwa sasa kimepatiwa majawabu kwa serikali ambapo tayari imetoa fedha na mkandarasi yupo eneo la mradi kwa ajiili ya ujenzi huo.
Nao baadhi ya wananchi wa Kata ya Igima, kijiji cha Mbingu wameishukuru serikali kwa kujenga barabara hiyo kwakuwa itaharakisha maendeleo yao ya kijamii na kiuchumi hasa usafirishaji wa uhakika wa mazao hasa mpunga (mchele) na ndizi .
Walisema kukamilika kwa ujenzi wake kutapunguza gharama za usafiri na usafirishaji wa mazao hayo kwenda kwenye masoko ya mjini na kuongeza kwa thamani ya mazao ya wakulima fofauti na sasa kutokana na kuwepo changamoto za miundombinu ya barabara.