MCC Asas: “Msiogope, tarehe 29 amani, kapigeni kura

IRINGA: MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Salim Abri ‘Asas’, amewahakikishia Watanzania kuwa uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29 utakuwa wa amani na utulivu, na kuwataka wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura bila hofu.
Akizungumza katika mkutano wa kufunga kampeni za Ubunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, uliofanyika katika kata ya Isalavanu, tawi la Ugute, mbele ya maelfu ya wananchi, Asas alisema serikali imejipanga vyema kulinda amani ya nchi wakati wote wa uchaguzi.
“Ndugu zangu, msiwasikilize wanaotisha mitandaoni. Serikali imejipanga vyema kudumisha amani. Oktoba 29 nendeni kwa amani, mpige kura zenu bila woga huu ni uchaguzi wa amani na utulivu,” alisema Asas huku akishangiliwa na umati wa wananchi.
MCC Asas aliongeza kuwa, badala ya kuongozwa na hofu, wananchi wanapaswa kutumia siku hiyo kuchagua viongozi wanaoamini katika maendeleo, utulivu na umoja wa taifa, akiwataka wakipe kura Chama Cha Mapinduzi kuanzia ngazi ya urais, ubunge hadi udiwani.

“Rais wetu Dk Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa isiyopingika. Kazi zake zinajitosheleza kumpa kura za kishindo. Oktoba 29 tumpatie zawadi ya kura nyingi kama shukrani kwa uongozi wake wa hekima,” alisisitiza.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Mafinga Mjini kupitia CCM, Dickson Lutevele, alisema maendeleo yaliyotekelezwa chini ya uongozi wa Rais Dk Samia ni uthibitisho kuwa wananchi wanapaswa kuendelea kuiamini CCM.
“Tuna kiu ya maji, elimu bora, huduma bora za afya na uchumi unaokua. Nikipewa dhamana, nitapambana kuhakikisha haya yanatekelezwa kwa vitendo,” alisema Lutevele.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Tanzania limetoa taarifa rasmi likiwahakikishia wananchi kuwa hali ya usalama nchini ni shwari, na kwamba hakuna tishio lolote litakaloweza kuvuruga uchaguzi huo.
Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime leo, imeeleza kuwa jeshi limejipanga kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu katika maeneo yote nchini.
“Wananchi mnahakikishiwa usalama wa kutosha. Nendeni mkapige kura bila hofu yoyote. Tutadhibiti kwa mujibu wa sheria yeyote atakayejitokeza kuhatarisha amani ya nchi,” alisema Misime.
Taarifa hiyo imehitimisha kwa kusisitiza kuwa Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayevunja sheria siku ya uchaguzi au baada yake.



