Salim Asas apiga kura, apongeza uchaguzi amani

IRINGA: Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Salim Asas, leo amepiga kura katika kituo cha Chuo cha Afya kilichopo kata ya Gangilonga, Manispaa ya Iringa, na kuipongeza jamii ya Iringa na Watanzania kwa ujumla kwa namna wanavyoshiriki uchaguzi huo wa amani, utulivu na heshima.
Akizungumza mara baada ya kupiga kura, Asas alisema kuwa hali ya uchaguzi ni shwari kabisa, na kwamba anaiona Tanzania ikiendelea kuwa mfano wa kuigwa katika siasa za kidemokrasia barani Afrika.

“Nimepiga kura yangu kwa utulivu mkubwa. Zoezi linaenda vizuri sana, hakuna vurugu, hakuna maneno mabaya. Huu ni ushahidi kwamba taifa letu limekomaa kisiasa na Watanzania wanathamini amani kuliko kitu chochote,” alisema Asas.
Aliongeza kuwa kwa mara ya kwanza katika historia ya chaguzi nchini, kumekuwa na utulivu wa hali ya juu, huku akiwataka wananchi wote kuendelea kujitokeza kwa wingi kutekeleza haki yao ya kikatiba kwa amani na upendo.

“Tuna muda hadi jioni. Kila mtu ajitokeze kupiga kura bila woga, kwa sababu usalama upo wa kutosha. Tukimaliza tutarudi majumbani tukiwa tumetimiza wajibu wetu kwa nchi yetu,” alisisitiza.
Katika kituo cha Chuo cha Afya, wananchi wa rika mbalimbali walionekana wakifika kwa wakati, wakiwa na mstari wa nidhamu tangu asubuhi. Wengine waliopiga kura katika kituo hicho ni Balozi, Dk Pindi Chana, na viongozi wengine waandamizi wa CCM.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, alisema hali ya usalama katika mkoa huo ni tulivu na thabiti, akiwahakikishia wananchi kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vipo kazini kuhakikisha kila kitu kinaenda kwa amani.

“Zoezi linakwenda vizuri, watu waendelee kujitokeza kupiga kura kwa utulivu. Kura zitahesabiwa kwa usalama na matokeo yatatangazwa kwa usalama. Niwasisitize tusibomoe amani tuliyoijenga kwa miaka mingi,” alisema RC James.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Zaina Mlawa, aliwapongeza maafisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) akisema wanatekeleza majukumu yao kwa weledi mkubwa, na wananchi wameonyesha nidhamu ya hali ya juu katika vituo mbalimbali vya kupigia kura.
Zoezi hilo la Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, linahusisha kuwachagua viongozi katika ngazi mbalimbali za uongozi, wakiwemo Madiwani, Wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ulinzi uliimarishwa ipasavyo, huku askari wakihakikisha kila kitu kinaenda kwa utulivu na amani, jambo linalotoa taswira chanya kwa taifa zima kuwa Tanzania bado ni ngome ya amani, umoja na demokrasia ya kweli.



