Mfuko waja kuwezesha wajasiriamali wadogo

DODOMA – SERIKALI imelieleza Bunge kuwa itaanzisha utaratibu wa Mfuko wa Mtaji (VCF), ili kutoa mtaji kwa biashara zinazoanza na ndogondogo kwa utaratibu utakaowekwa.

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alisema hayo bungeni Dodoma juzi wakati akiwasilisha mapendekezo ya serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Dk Mwigulu alisema pia serikali imeandaa mkakati wa kuongeza ushiriki wa wazawa katika utekelezaji wa miradi.

Advertisement

Aliwaeleza wabunge kuwa serikali itafanya marekebisho katika Sheria ya Ununuzi wa Umma Namba 10 ya Mwaka 2023 kwa kuongeza wigo wa thamani ya miradi ya kutekelezwa na wazawa peke yao.

“Nitoe rai kwa sekta zote kuhakikisha kuwa zinazingatia sheria hiyo na pia mikataba inayosainiwa na makampuni ya nje ihakikishe inazingatia sera ya uwezeshaji ikiwemo kutumia huduma na rasilimali zinazopatikana hapa nchini pamoja na kutoa ajira za moja kwa moja kwenye utekelezaji wa miradi husika,” alisema Dk Mwigulu.

Aliongeza: “Uwezeshaji wa wazawa utaleta manufaa ikiwemo faida inayopatikana kutokana na utekelezaji wa miradi kubaki nchini na kutumika kukuza biashara za wazawa; kupunguza matumizi ya fedha za kigeni; kuongeza ajira na ujuzi kwa wataalamu wa ndani pamoja na kujenga uwezo wa kampuni za ndani kuweza kushindana kimataifa”.

Serikali inatenga kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, lakini sehemu kubwa ya fedha hizo haziwanufaishi wazawa ipasavyo.

SOMA: Dk Mwinyi ateua kamishna, wakurugenzi

Dk Mwigulu alisema sababu kubwa zinazochangia kuwepo kwa hali hiyo ni uwezo mdogo wa kifedha kwa makandarasi wa ndani, mitambo na wataalamu ikilinganishwa na kampuni za nje.

“Serikali imedhamiria kuwawezesha makandarasi wazawa kushiriki kwenye kazi kubwa za ujenzi katika hatua na taratibu zote kuanzia mipango, usanifu, ununuzi, ujenzi na ukarabati,” alieleza Waziri wa Fedha.

Wakandarasi wageni kubanwa Dk Mwigulu alisema kumekuwa na utaratibu inaposainiwa mikataba na wageni inawekwa kwenye mkataba muda wa kulipwa hati za madai zilizoiva na ikichelewa hata siku moja inatengeneza riba.

Alisema hata hivyo mikataba hiyo haioneshi wajibu wa makandarasi hao kulipa riba watakapochelewesha malipo ya makandarasi wazawa walio chini yao hivyo serikali inakuwa na shinikizo la kuwalipa wageni fedha ambazo wao wanapitisha hata miezi minne mpaka sita bila kuwalipa wazawa.