JUBA : CHAMA cha Upinzani cha SPLM-IO nchini Sudan Kusini kimeingia kwenye mgogoro mpya wa uongozi kufuatia kuwekwa kizuizini kwa mwenyekiti wake Dkt. Riek Machar, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais. Kundi la viongozi waandamizi limetangaza kumteua Stephen Par Kuol kuwa kiongozi wa mpito hadi Machar atakapofunguliwa.
Par alisema hatua hiyo inalenga kutatua mgogoro uliosababishwa na kukamatwa kwa Machar pamoja na kutoweka kwa baadhi ya viongozi wa juu wa chama. Hata hivyo, uteuzi huo umezua mvutano, huku baadhi ya wajumbe wakipinga na kudai kuwa wanafanya mapinduzi ya kisiasa.
Umoja wa Mataifa umeonya kuwa hali ya sasa inaweza kuirejesha nchi hiyo kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe, licha ya makubaliano ya amani ya 2018 kati ya Machar na Rais Salva Kiir yaliyomaliza mapigano yaliyosababisha vifo vya takribani watu 400,000.