Mgombea urais TFF aomba uchaguzi usimamishwe

DAR ES SALAAM; MGOMBEA urais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Shija Richard anatarajia kuwasilisha barua rasmi Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF, akiomba mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa shirikisho hilo usitishwe hadi hapo haki itakapotendeka.

Uchaguzi Mkuu wa TFF unatarajiwa kufanyika Agosti 16, mwaka huu na tayari wagombea mbalimbali wamechukua fomu na kurejesha huku baadhi yao akiwemo Shija wakidai wamekosa udhamini.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, mgombea huyo anadai kuwa mgombea mwenzao amekiuka katiba ya TFF na kanuni za uchaguzi kwa kujihakikishia wadhamini 46 kati ya 47,  hali iliyofanya wagombea wengine kushindwa kufikia idadi ya wadhamini wanaotakiwa ambao ni angalau watano.

“Tukisema tuendelee na uchaguzi tafsiri yake ni kwamba kuna mtu ataingia kwenye uchaguzi akiwa mgombea pekee, kitendo ambacho amenajisi uchaguzi,”amesema.

Amesema zoezi za uchaguzi linapaswa kurudiwa upya lifanyike katika mazingira ambayo wadhamini watakuwa huru na wagombea wote washiriki uchaguzi mkuu.

“Kanuni za uchaguzi za mwaka 2021 ambazo ndio zinafanya kazi hivi sasa zinaelekeza kwamba mgombea wa nafasi ya urais anatakiwa kupata udhamini wa taasisi zisizopungua tano ambazo ni wadau kwa mujibu wa Katiba ya TFF. Ni vyama vya mikoa ambavyo viko 26, klabu za Ligi kuu 16 na vyama shiriki vitano,”amedai

Mbali na kuomba uchaguzi usitishwe kupitia BMT, mgombea huyo amesema anapanga kuwasilisha malalamiko rasmi kwa Kamati ya Maadili ya TFF  na Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi, akitaka kutenguliwa kwa mchakato wa udhamini uliofanyika nje ya utaratibu wa kikatiba.

Shija ambaye aliwahi kuwa mjumbe wa kamati ya Utendaji Yanga, amesema wakati anapambana kupata udhamini alikuta wadhamini 46 kati ya 47 wameshachukuliwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button