Mgombea urais UMD aahidi elimu, afya bora

DAR ES SALAAM: Mgombea urais kupitia chama cha UMD, Mwajuma Mirambo, ameendelea na kampeni zake za kunadi sera za chama hicho leo jijini Dar es Salaam, katika Wilaya ya Ilala, Jimbo la Segerea, kata ya Vingunguti, kwenye uwanja wa Msikate Tamaa.

Akizungumza mbele ya wananchi waliojitokeza kwa wingi, Mirambo amesema serikali ya UMD ikipewa ridhaa ya kuongoza, itazingatia kuboresha mazingira ya sekta ya elimu kwa kuhakikisha walimu wanathaminiwa na kuwekewa mazingira rafiki ya kufanyia kazi.

“Tutahakikisha tunamjali mwalimu ili naye awe na moyo wa kuwalea wanafunzi kwa upendo. Tukimthamini mwalimu, tutaongeza hamasa ya wanafunzi kupenda shule kwa sababu mazingira yatakuwa rafiki,” alisema Mirambo.

Aidha, akizungumzia sekta ya afya, Mirambo aliahidi kuwa serikali yake itahakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa wananchi wote, huku huduma kwa mama na mtoto zikitolewa bure, akisisitiza kuwa rasilimali zilizopo nchini zinatosha kutimiza lengo hilo.

“Hatutaki kuona tena akinamama wanapoteza maisha kwa kukosa pesa ya matibabu. Serikali yetu itahakikisha huduma hizo zinapatikana bure,” aliongeza.

Katika mkutano huo wa kampeni, wananchi wa Vingunguti walimshangilia mgombea huyo huku wakionesha matumaini kuwa sera anazozinadi zinaweza kuleta mabadiliko chanya kwa Watanzania wengi.

Mirambo aliwahimiza wananchi kuendelea kudumisha amani wakati wa kipindi chote cha kampeni na kuwaomba wajitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura ili kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo ya kweli.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button