Mifugo, uvuvi inachangia 6% pato la taifa – Dk Nchimbi

SUMIYU: KATIBU wa Mkuu Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel Nchimbi amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi inachangia asilimia 6 ya pato la taifa.
Kufuatia hatua hiyo, Dk Nchimbi ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mabadiliko yaliyochochea mafanikio hayo kwa kipindi cha miaka minne.
Katibu Mkuu huyo amesema hayo leo Juni 14, 2025 aliposhiriki kongamano kubwa la wafugaji uwanja wa Kabindi uliopo wilayani Bariadi mkoani Simyu ambapo ameshirikiana na maelfu ya wafugaji kujadili kwa pamoja maendeleo ya mifugo nchini.
SOMA ZAIDI
Amesema kuwa kwa miaka mingi wizara hiyo ilikuwa haina mchango mkubwa katika taifa lakini kwa kipindi cha miaka minne pekee wizara hiyo imeonyesha mabadiliko chanya na sasa wizara inachangia.
Amesema mabadiliko hayo yanatokana na serikali kupandisha bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoka Sh bilioni 66 hadi bilioni 400 ambapo amewahakikishia wafugaji kuwa wategemee mabadiliko makubwa katika sekta ya mifugo.
“Nakupongeza waziri kwa mabadiliko makubwa sana katika sekta hii ,kwa muda mchache umefanya mabadiliko na ubunifu mkubwa na sasa kuna mabadiliko makubwa katika sekta ya uvuvi hasa upanuaji wa masoko ufugaji wenye tija na miaka mitano ijayo tutashuhudia mabadiliko makubwa zaidi,” amesema Dk Nchimbi.
Kupitia kongamano hilo alitaka maamuzi ya mahakama kuhusu wafugaji walioshinda kesi za mifugo yao kukamatwa ifanyiwe kazi haraka na ofisi ya waziri mkuu ili wafugaji hao walipwe fidia.
Ametoa wito kwa wafugaji kufuata sheria na kujiepusha na migogoro kwani tayari serikali imemaliza migogoro yote ya wakulima na wafugaji.
Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Ashatu Kijaji amesema kuwa mipango ya sasa na mikakati wizara hiyo utachangia pato la taifa asilimia 10 kufikia 2030.
Amesema kwa sasa mipango ya serikali kuhakikisha wafugaji wanamiliki ardhi zao na kupanda malisho yao inafikiwa kikamilifu huku akidai kuwa miaka 10 ijayo wizara itatengeneza mabilionea 10 wanaotokana na ufugaji.