“Mikakati ya Serikali ni kuinua pato la mtu mmoja mmoja”

GEITA: MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulurhaman Kinana amesema mkakati wa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ni kuinua pato la mtu mmoja mmoja kupitia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 -2050.

Akizungumza katika Mkutano wa wananchi wa Jimbo la Chato mkoani Geita, leo Desemba 12, 2023 Kinana amesema kuwa Desemba 9, 2023 Rais Samia amezindua Mpango wa Dira ya Taifa ya Maendeleo.

“Kwa wale ambao hamkusikiliza nitamshauri Katibu Mkuu (Ikulu) achukue zile dondoo zilizotolewa na Waziri wa Mipango Profesa, Kitila Mkumbo ampelekee kila mjumbe kwenye Whatsapp yake ili wajue kazi iliyofanyika.

“Tulianza na dira ya miaka 25, iliyoanza mwaka 2000 hadi mwaka 2025, sasa tunaandaa nyingine ya 2025/2050 ukisikiliza kwa makini ile dira ya 2020/2025 kila kitu kilichopangwa tulichodharimia, tulichoahidi kimetekelezwa kwa zaidi ya asilimia 85.

“Kuanzia miradi ya maji , elimu, afya, ujasiriamali , miundombinu , umoja, amani , demokrasia , mshikamano , uwekezaji, kila jambo lililopangwa katika dira ya 2020/2025 limefanyika.Sasa tunajiandaa kwa nafasi nyingine,”amesema.

Amesema anaamini katika miaka 25 ijayo serikali itaendelea kuimarisha mambo hayo yanayozungumzwa kila siku ya elimu , afya , miundombinu lakini na mkazo utawekwa katika kukuza pato la kila mtu kwa maana ya pato binafsi.

“Pato binafsi litakuzwa kwa kutumia mbinu na njia mbalimbali.Wakati mwingine wananchi wanalalamika, sasa mimi kwa umri wangu nimesikiliza sana malalamiko ya wananchi, sehemu kubwa ya malalamiko yanatokana na maendeleo.

“Wananchi wakipata maji , wanataka kitu kingine , kwa hiyo maendeleo makubwa yanafanya wakati mwingine malalamiko yawe makubwa. Nakumbuka miaka ya kwanza ya uhuru wa nchi yetu miaka ya 1970,1980 kulikuwa hamna malalamiko kwasababu maisha yalikuwa ya kawaida,”amesema.

Amefafanua wakati huo ukizungumzia barabara hazipo, maji hayapo, shule za kawaida na miundombinu ya chini,hivyo hakukua na malalamiko kwasababu huwezi kulalamika kwa kitu ambacho hujakiona.

“Sasa kila ukipiga hatua unataka hatua zaidi, kwa hiyo wakati mwingine kelele tunazosikia hizi sio lawama, ni za kutuambiwa sawa tunawashukuru sana, kwa haya mliyofanya lakini tumepata hamu kubwa zaidi ya kupata mengine mengi zaidi.

“Wananchi wanasema maji tumepata uongezeni zaidi wapate maji nyumbani.
Tulikuwa na umeme kila Wilaya, baadae kila kata, sasa wananchi wanataka kila kitongoji, kwa hiyo ni kelele nzuri tu , ni madai mazuri, watu wanataka maendeleo,”amesema Kinana.

Amepongeza hivi sasa kuna barabara za lami zinazounganisha mkoa na mkoa, wilaya na wilaya na matokeo yake wananchi wanataka barabara katika vitongoji na mitaa yao.”Sio kwamba wanalalamika bali wanakata maendeleo zaidi.

“Baba wa taifa alituambia kupanga ni kuchagua, kwa hiyo kazi kubwa tuliyonayo ni kuongeza mapato ya nchi yetu ili yaweze kukidhi mahitaji.

Habari Zifananazo

Back to top button