Milioni 2 wanufaika na Kampeni ya Mama Samia ya Msaada wa Kisheria

DAR ES SALAAM — Kampeni ya Mama Samia Legal Aid, iliyoanzishwa mwaka 2023 kwa lengo la kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi, imewafikia na kuwahudumia zaidi ya wananchi milioni 2 nchini kote. Kampeni hiyo sasa inatua rasmi jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 16 hadi Juni 25, 2025.
Kampeni hii ni matokeo ya ushirikiano kati ya Wizara ya Katiba na Sheria na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, chini ya udhamini wa Rais Samia Suluhu Hassan. Uzinduzi rasmi utafanyika Juni 16, 2025, katika uwanja wa Maturubai, Mbagala – Wilaya ya Temeke, na utaongozwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya kampeni hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewahimiza wakazi wa jiji hilo kujitokeza kwa wingi ili kupata huduma za msaada wa kisheria bure. Ameeleza kuwa kampeni hiyo inalenga kutatua changamoto mbalimbali kama vile migogoro ya ardhi, ukatili wa kijinsia, na masuala mengine ya kisheria ambayo yanawakumba wananchi wa hali ya chini.
“Tunawakaribisha wakazi wote wa Dar es Salaam, hasa wale wenye changamoto za kisheria. Kupitia kampeni hii, watapata fursa ya kusikilizwa na kusaidiwa na wataalamu wa sheria na madawati ya kijinsia. Hii ni jitihada ya Rais Samia kuhakikisha haki inapatikana kwa wote,” amesema Chalamila.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Ester Msambazi, amesema tangu kampeni hiyo ianze mwaka 2023, tayari imefika katika mikoa yote mitano ya Zanzibar na mikoa 25 ya Tanzania Bara. Kwa ujumla, watu zaidi ya milioni 2 wamepokea msaada wa kisheria katika maeneo mbalimbali kupitia huduma hii.
Bi. Msambazi amesema kampeni hiyo imejikita katika kuhakikisha kuwa huduma za kisheria zinawafikia wananchi moja kwa moja katika maeneo yao ya karibu, bila gharama yoyote, na kuongeza usawa katika upatikanaji wa haki.
Baada ya uzinduzi wa Dar es Salaam, kampeni hiyo itaendelea kutolewa katika wilaya zote za mkoa huo, ambapo huduma zitatolewa na wataalamu wa sheria, madawati ya kijinsia, na watoa huduma za kijamii kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za haki jinai na za kiraia.
