NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema ifikapo mwaka 2030 watu milioni 300 Afrika watakuwa wanatumia nishati safi ya kupikia.
Amesema juhudi zinazofanyika katika kufikia lengo hilo zimepelekea Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Benki ya Dunia (WB) kuunga mkono Ajenda ya nishati safi ya kupikia Afrika.
Dk Biteko ameyasema hayo alipozungumza katika mkutano wa siku mbili kuhusu majadiliano ya masuala ya nishati kwa Bara la Afrika kwa ngazi ya mawaziri unaofanyika Dar es salaam kwa siku mbili.
SOMA: Majaliwa azindua benki ya TADB Kanda ya Kusini
Amesema AfDB imeichangua Tanzania kufanya mkutano huo wa majadiliano ikiwa Tanzania inazidi kupiga hatua kubwa ya mafanikio katika sekta ya nishati.
“Mkutano huu pia ni sehemu ya maandalizi ya mkutano wa marais wa nchi za Afrika unaotarajiwa kufanyika mwaka 2025 ikiwa ni mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye kinara wa ajenda ya Nishati safi ya kupikia Afrika,” amesema Dk Biteko.
Ameongeza kuwa, mkutano huo utafanya tafakuri na utaweka mikakati ya kuhakikisha kuwa nishati safi ya kupikia inapatikana kwa uhakika na gharama nafuu.