WIZARA ya Ujenzi kupitia Wakala wa barabara (TANROAD) Mkoa wa Kagera imemabidhi mkandarasi Shandong Luqiao Group kazi ya utekelezaji wa barabara kiwango cha lami Kyerwa Omurushaka kilometa 50 itakayogharimu shilingi Sh bilioni 94.34.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashingwa amesema ujenzi wa barabara hiyo unaendelea kuweka mazingira wezeshi katika kuzalisha mali pamoja na kuchochea utalii Kagera kupitia hifadhi za taifa za Ibanda Kyerwa na Rumanyika Karagwe.
Amesema serikali inatambua mchango mkubwa wa Halmashauri ya Kyerwa katika swala la uzalishaji wa mazao na kusema kuwa serikali inaendelea kuhakikisha miundombinu inakuwa wezeshi ili wananchi waendelea kuzalisha kwa wingi.
Amesema mradi huo wa Rwenkorongo Omrushaka ambao umekabidhiwa kwa mkandarasi inatakiwa kukamilika June 2027 kwa lengo la kuwawezesha wananchi katika miundombinu hiyo ya barabara huku akimtaka mkandarasi kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kwa wakati.
“Pamoja na kilomita 50 ambazo zitaanza kutekelezwa kuanzia Rwenkorongo pia serikali imeongeza kilomita 11 ili kukamilisha barabara ya kuanzia Chonyonyo hadi Omrushaka natoa wito kwa wananchi waitumie fursa hiyo katika shughuli za maendeleo na kuinua uchumi kwani miundo mbinu ya barabara itakua wezeshi,”amesema Bashingwa.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Fatma Mwasa katika hafla hiyo ya makabidhiano amemuomba Waziri wa Ujenzi kusaidia Halmashauri ya Kyerwa kukamilisha vipande vya miradi ya barabara ya lami vilivyobakinili kuiweka wilaya hiyo katika ramani ya taifa.