Mkonge kuwafungulia neema wakulima Tanga

ZAIDI ya wakulima wa mkonge 5,000 mkoani Tanga watanufaika kwa kupata soko la uhakika la mazao yao na bei bora hatua inayotarajiwa kuinua hali yao ya kiuchumi kupitia mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kisasa cha kuchakata mkonge unaotekelezwa na Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), katika Kijiji cha Taula Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.

Aidha, mradi huo uliogharimu zaidi ya Sh milioni 710, pia utazalisha ajira za moja kwa moja kwa wafanyakazi wapatao 150 huku wafanyabiashara wadogo na wa kati wakipanua biashara zao kwa kutoa huduma mbalimbali kwa kiwanda na wafanyakazi wake.

Hali hiyo inaelezwa kuwa itachochea ukuaji wa biashara katika eneo hilo. Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TSB, Profesa Esther Dungumaro anabainisha hayo wakati wajumbe wa bodi hiyo walipotembelea mradi huo na kujionea ujenzi unaoendelea sanjari na kutembelea Shamba la Mkonge la Kibaranga wilayani Muheza linaloendelea na uboreshaji wa miundombinu ya uchakataji mkonge na Shamba la Ufugaji la Mruazi.

Anasema wakulima wa mkonge watanufaika kwa kuwa na sehemu ya uhakika wa kuchakata mkonge baada ya serikali kuanza utekelezaji wa uwekaji wa mashine za kusindika (korona) katika maeneo mbalimbali yanayolima mkonge nchini.

Ufungaji wa mashine hizo za kisasa za kuchakata zao ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu
Hassan kuhakikisha wanamaliza changamoto inayowakabili wakulima wadogo wa mkonge ya uhaba wa
mashine hizo kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Profesa Dungumaro anasema maboresho kama hayo yanaendelea katika sehemu mbalimbali nchini yakianzia mkoani Tanga na kuendelea katika mikoa ya Pwani, Morogoro pamoja na ile ya Kanda ya Ziwa na maeneo mengine yaliyohamasika kulima zao hilo.

“Handeni ni eneo mojawapo ambalo tunajenga kiwanda cha kuchakata mkonge. Ikumbukwe Serikali ya Awamu ya Sita imehamasisha sana wakulima wa mkonge miaka mingi iliyopita zao hili lilikuwa linaibeba nchi yetu kitaifa na kimataifa,” anasema.

Anaongeza: “Kwa sasa kwa busara za Rais Samia Suluhu Hassan umefanyika uhamasishaji kwa wakulima wa mkonge, lakini changamoto tunayokutana nayo ni viwanda vichache vya uchakataji. Hivyo, Rais Samia alitoa agizo viwanda vijengwe ili kuwasaidia wakulima wadogo kuchakata mkonge wao.”

“Kwa hiyo, sisi kama bodi tukishirikiana na Menejimenti ya TSB na Waziri wa Kilimo, tumeanza kutekeleza ujenzi wa viwanda vya kuchakata mkonge tukianzia hapa Handeni lakini tutakwenda, Lushoto, Korogwe na Mkinga,” anasema na kufafanua kuwa, mradi huo haujalenga kutatua tu changamoto za wakulima wadogo, bali pia kwa ukubwa wake utatengeneza fursa za ajira nchini.

Kwa mujibu wa Dungumaro, hatua hizo ni utekelezaji wa agizo la Rais kwamba, miundombinu iboreshwe na wakulima wadogo wapate fursa ya kuchakata mkonge wao.

“Kwa hiyo kama Makamu Mwenyekiti, nampongeza Rais na kumueleza kuwa tumetekeleza maagizo yake kwa vitendo na tunakoelekea tutahakikisha changamoto za mitambo na viwanda vya uchakataji mkonge zinaisha na viwanda vingine vitajengwa katika mikoa mingine,”amesema.

Akizungumzia shamba la Kibaranga, Profesa Dungumaro anasema kinachofanyika sasa ni uboreshaji katika eneo la ukarabati wa mashine ya kuchakata mkonge. “Tunaishukuru serikali si tu kwamba wakulima wadogo watafaidika kwa kuhakikisha mkonge wao hauharibiki na unachakatwa kwa wakati na pia unaongeza ajira,” anasema.

Mkurungenzi wa Bodi ya TSB, Saddy Kambona anasema bodi hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, imeweka mpango wa kuanzisha vituo vya usindikaji ili kusaidia mkulima mdogo kusindika na kupata singa (nyuzi) zenye ubora unaokubalika katika soko la ndani na nje ya nchi.

“Moja ya changamoto inayowakabili wakulima wadogo wa mkonge ni uhaba wa mashine za usindikaji hivyo tayari sisi kama bodi, tumewekeza zaidi ya Sh bilioni moja kwa ajili ya ukarabati na uwekaji wa mashine za kisasa katika maeneo ya wakulima wa zao hilo,” anasema Kambona.

Anasema mikakati ya bodi hiyo ni pamoja na kuhakikisha wakulima wadogo wananufaika na kilimo hicho
kutokana na hamasa kubwa inayoshafanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau wa zao hilo. Hivyo kupitia uwekezaji huo, anasema wataongeza thamani ya mkonge na kuwaondolea wakulima changamoto za uhaba wa
mashine za kuchakata zao hilo ili wafikie ongezeko la uzalishaji wa zao hilo.

Anasema, “Mwaka 2020 uzalishaji wa zao la mkonge ulikuwa tani 26,000 na mpaka sasa baada ya uhamasishaji uzalishaji umeweza kuongezeka hadi kufikia tani 61,000 hivyo kutokana na uwekaji wa mashine mpya za kisasa, tuna imani hadi mwishoni mwa mwaka huu malengo ya serikali ya kufikisha tani 120,000 yanaweza kufikiwa.”

Anasema bodi kwa kishirikana na Wizara ya Kilimo itaendelea kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima wa mkonge sambamba na kuongeza hamasa ya kilimo cha zao hilo.

“Mkonge una soko kubwa sasa kimataifa hivyo wajibu wetu bodi kwa kushirikiana na serikali na sekta binafsi kuhakikisha tunawajengea uwezo wakulima wetu ili wazalishe mkonge wenye ubora utakaotupatia singa ambazo zitauzika kwa urahisi katika masoko ya dunia,” anasema Kambona.

Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa wa Kijiji cha Taula, Zaina Mohamed anasema ujenzi wa kiwanda hicho ni mkombozi wa kijiji hicho kwani licha ya wakulima kufaidika, vijana wa kijiji hicho na maeneo jirani pia wamefaidika kwa ajira.

“Nikiwa kama mwenyekiti nimepambana kuhakikisha na sisi hapa tunakuwa na uwezo wa kusema ‘nakwenda kazini’ kwa sababu awali tulikuwa tunakwenda kufanya kazi katika vijiji vingine na watoto wetu walikuwa wakimaliza shule wanakwenda kutafuta ajira Dar es Salaam lakini kwa mradi huu watatulia hapa kijijini,” anasema.

“Tunamuomba rais kama kuna mradi mwingine, Taula tuko tayari tuna maeneo ya kutosha,” anaongeza. Mwenyekiti Chama cha Ushirika cha Kibaranga (Kibaranga Amcos), Paulo Haule anasema kwa ukarabati unaoendelea licha ya ajira, pia utawaingizia kipato kwani wakulima wa Muheza na majirani zao ambao ni
Wilaya ya Mkinga watapata fursa ya kupeleka mkonge wao badala ya kupeleka maeneo mengine.

“Tunamshukuru Rais kwa kutuwezesha sisi wakulima wadogo kupata viwanda kama hivi na kukarabati
kiwanda chetu ili hatimaye wananchi waweze kuboresha maisha,” anasema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button