Wagonjwa wa figo kuchujwa damu Mlongazila

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili–Mloganzila imeandaa kambi maalum ya kutengeneza na kurekebisha mishipa ya kuchuja damu kwa wagonjwa wenye changamoto za figo ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha upatikanaji wa huduma bora na salama za kuchuja damu.
Akizungumza jijini Dar-es-salaam kuhusu kambi hiyo ambayo inayotarajia kuanza Februari 14 hadi 18,Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Mishipa ya Damu, Dk David Antanamsu amesema kambi itahusisha wataalamu bingwa wa ndani ambapo wagonjwa ambao bado hawajawekewa mishipa ya kuchuja damu pamoja na wale waliowekewa kwa muda mrefu lakini mishipa hiyo imeshindwa kufanya kazi.
Amesema utengenezaji na urejeshaji wa mishipa ya kuchuja damu una faida nyingi ikiwemo kupunguza hatari ya maambukizi, kuongeza muda wa matumizi ya mshipa pamoja na kupunguza gharama za kubadilisha mpira wa kuchuja damu (catheter) mara kwa mara. Dk Antanamsu amebainisha kuwa hatua hiyo huchangia kuboresha afya na ubora wa maisha ya wagonjwa wenye figo kushindwa kufanya kazi. SOMA: Mlongazila yaondoa mawe bila upasuaji
Kupitia kambi hiyo, Hospitali ya Taifa Muhimbili–Mloganzila inaendelea kuimarisha utoaji wa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi kwa kuanzisha huduma bunifu zenye tija kwa jamii pamoja na kuunga mkono jitihada za Serikali za kusogeza huduma za afya karibu na wananchi kwa kuzingatia ubora, usalama na ufanisi wa huduma zinazotolewa.



