Molly Sims awakumbuka watoto njiti

MWANAMITINDo na Mwigizaji wa Kimataifa Molly Sims amechangia Dola za Marekani 25,000 sawa na sh milioni 62 kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa watoto njiti katika hospitali ya Kwinba mkoani Mwanza.
Molly ambaye ni mke wa Mwenyekiti wa Netflix Films, Scott Stuber, yupo nchini Tanzania kwa ajili ya kampeni ya ujenzi wa wadi za watoto njiti.

Molly amechangia pesa hizo akiwa ni kuunga mkono jitihada za Doris Mollel Foundation ambao wamekuwa wakijihusisha na masuala ya watoto njiti.
Ujio wa mwanamitindo huyo umefanikishwa na Taasisi ya Kimataifa ya JHPIEGO.
Ufunguzi wa kampeni hiyo umeudhuriwa na Mkuu wa Idara ya Mama na Mtoto na Afya ya Uzazi wa Wizara ya Afya, Dkt. Felix Bundala pamoja na Viongozi kutoka Makao Makuu ya JHPIEGO duniani.

Mkurugenzi wa Doris Mollel Foundation, Doris Mollel na Mkurugenzi Mkazi wa JHPIEGO Tanzania Alice Christensen kwa pamoja wameahidi kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo kushawishi wadau wengine na serikali kuchangia fedha nyingine za kumalizia jengo hilo.
Itakumbukwa Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan alichangia pesa zake binafsi sh milioni 70 kwa ajili ya kutoa hamasa ya ujenzi pamoja na kununua vifaa vya watoto njiti katika Hospitali hiyo ya Wilaya ya Kwimba mwaka jana kwenye maadhimisho ya siku ya Mtoto Njiti duniani .