Mongella ataka viongozi wanyenyekevu

MWANASIASA mkongwe nchini, Balozi Getrude Mongella amewataka viongozi wawe wanyenyekevu kwa wenzao na wananchi wanaowaongoza.
Pia Mongella amewasihi viongozi wazingatie maadili na wawe wepesi kujifunza kutokana na mazingira.
Ameyasema hayo nyumbani kwake Makongo Juu wilayani Kinondoni mkoani Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) hivi karibuni.
Balozi Mongella alisema malezi ya wazazi wake ya kutoficha kipaji chake na juhudi ya kujifunza kutokana na mazingira, vimemjenga na kumfanya kuwa kiongozi anayejiamini, kuthubutu na mpambanaji katika maisha yake.
Alisema dalili za yeye kuwa kiongozi zilianza kujitokeza mapema tangu akiwa mdogo kutokana na kujikuta akitangulizwa mbele katika mambo mbalimbali ya kiuamuzi na kujikuta akitegemewa kutoka kwa watu wanaomzunguka bila kujua kuwa wenzake wameshajua kipaji chake cha kuongoza.
Balozi Mongella alisema mtoto anakuzwa kwa kuendelezwa vipaji vyake na wazazi wake pamoja na majirani zake huku jamii inayomzunguka ikiwa mfano bora kwake hususani katika kujitegemea, utunzaji na ufuatiliaji wa mila na desturi ndani ya jamii.
“Nilizungumza na mdogo wangu anayenifuata tukajikumbusha maisha ya zamani, nikamuambia kumbe mambo tuliyokuwa tunayaona kwa mama anatutajia wanawake pale kijijini wanaofanya kazi na kujitegemea na kusomesha watoto wao, nikaona kumbe uongozi mwingine tumejifunza kutoka kwa wanawake wa kijijini tulioishi nao,” alisema mwanasiasa huyu mkongwe.
Alisema mtu anapoishi katika jamii ya namna hiyo inamuimarisha kwa sababu mbali ya vipaji alivyonavyo, pia anapata kujifunza maarifa kutokana na wanawake au wanaume viongozi katika jamii katika ngazi ya chini kabisa.
Alisema viongozi wengi nchini wanakuwa na aina hiyo ya uongozi ambayo wapo walizaliwa nayo, lakini kwa namna moja au nyingine wakaimarishwa na mazingira wanayoishi ndani ya jamii katika maeneo yao.
Mbali na uongozi wa kuzaliwa kwa maana ya kipaji, Balozi Mongella alisema uwezo wake uliimarishwa kutokana na uongozi wa kujifunza kutokana na mambo anayoyafanya, akitolea mfano wakati alipokuwa Rais wa Bunge la Afrika ilibidi ajifunze kutoka Bunge la Umoja wa Ulaya na Amerika Kusini namna linavyofanya kazi.
“Uongozi wa namna hiyo unatakiwa kuwa mnyenyekevu na mwepesi wa kujifunza sio ujione unajua kila kitu, hivyo lazima ujue mbinu mbalimbali zitakazokufanya uongoze vizuri zaidi. Hakuna kitu kibaya zaidi kama kiongozi uonekane mpumbavu,” aliongeza waziri huyo wa zamani.
Alisema watu wengi wanafunika vipaji vyao vya kuongoza hususani wanawake, akisema inafikia anateuliwa kushika wadhifa fulani, lakini anakataa kutokana na hofu ya kuhofia kushindwa kutekeleza majukumu.
“Nimeyaona haya mimi mwenyewe nilipokuwa Ofisi ya Waziri Mkuu nilikuwa nashangaa na kuhoji mbona wakuu wa wilaya ni wachache…mwishowe Mwalimu (Baba wa Taifa) akasema tuletee orodha, mbona nilikaribia kushindwa kwa sababu kila ninayemgusa ateuliwe kuwa mkuu wa wilaya anakataa kwa nguvu zote,” alisema Balozi Mongella.
Alisema si kwamba wanawake hao walikuwa hawawezi kuongoza bali walizoea zile mila na desturi zilizokuwa zikiwadidimiza kuwa hawawezi masuala ya uongozi, lakini ukweli wanao uwezo na sifa za kuwa viongozi wanawake.
Alisema wanawake wengi vipaji vinakufa kutokana na kujawa na woga kutoka kwa jamii ambayo ilikuwa ikiamini kuwa mwanamume pekee ndiye anayeweza kutokana na kuwa na ujasiri hivyo kuwaacha wanawake wengi kuwa wategemezi.
“Mazingira ya zamani yalikuwa ni magumu kumjenga na kumwezesha mwanamke kuwa kiongozi, ilihitajika kujitutumua pamoja na aina fulani ya ujeuri usioudhi ili kuweza kuvuka mtego huo,” alisema.
Mfumo wa demokrasia
Balozi Mongella alisema anatamani mfumo wa demokrasia ya asili ambayo sio tu inasaidia katika utawala, bali pia inaweza pia kusaidia katika kuimarisha maadili ya Mtanzania.
Alisema matatizo mengi yanayoikumba jamii na taifa katika malezi na makuzi ya watoto yalianza pale demokrasia ya zamani ilipopewa kisogo na kugeukia demokrasia ya wazungu ambayo imeleta mambo yasiyofaa ndani ya jamii.
“Kwanini tusiwape nafasi vijana wetu wakaenda kufukua mifumo ya tawala za zamani katika jamii mbalimbali halafu tukatafuta humo maana, sifa na faida za demokrasia, badala yake tumetingwa kutafuta kwa Wamarekani na Uingereza,” aliongeza Balozi Mongella.
Alihoji kuwa kwanini maana ya demokrasia haitoki katika tawala za Kihaya, Kichaga, Kimakonde, Kikurya au Kipare kwa sababu humo hakuna uwezekano wa kupata jambo linaloenda kinyume na mfumo wa utawala wa nchi.
Aridhia Nyerere ang’atuke
Balozi Mongella alisema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alifundisha demokrasia nzuri ya kiongozi kuachia madaraka mapema akiwa na nguvu ili kuepusha viongozi wajao kung’ang’ania uongozi hadi kufia madarakani.
Alisema baada ya Mwalimu kuwasilisha hoja ya kung’atuka katika kikao cha Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kulitokea mgawanyiko wa kidemokrasia kwa kuwa baadhi wajumbe walikataa kumruhusu, lakini wengine akiwemo yeye walikubaliana na wazo lake kuwa wakati umefika aondoke madarakani.
“Nakumbuka tulikuwa katika kikao cha Kamati Kuu, Mwalimu anataka kuondoka madarakani na sisi tupo tumechachamaa tunataka abaki na tulikuwa tuna hoja mbalimbali. Mimi kwa kweli ni miongoni mwa wale waliosema aondoke,” alisema Balozi Mongella.
Alisema watu walimtazama kwa jicho baya, lakini aliwaeleza sababu kwa kuwa Mwalimu kipindi cha ujana wake wote alikitumia kazini kulitumikia taifa bila kuwa karibu na familia yake, hivyo ni vyema akatumie muda uliobaki kuwa karibu na familia yake.