Msaada wa kisheria wa Samia kuanza leo Mtwara

UTOAJI wa elimu ya kisheria kwa wananchi mkoani wa Mtwara kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Samia Legal Aid Campaign) utaanza Januari 24 hadi Februari 2 mwaka huu.

Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara, Bahati Geuzye amesema hayo leo wakati akizindua mafunzo ya utekelezaji wa kampeni hiyo kwa waratibu 100 kutoka halmashauri tisa za mkoa huo.

Mafunzo hayo kwa waratibu yamelenga kuwawezesha waratibu hao kuhudumia wananchi ambao wana uhitaji wa huduma za msaada wa Kisheria ili kuwasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

“Wananchi watakapokuwa na uelewa wa masuala ya kisheria itasaidia kuondoa migogoro iliyopo baina yao na kufuata taratibu rasmi za kisheria pale inapohitajika,” amesema.

Katibu Tawala huyo amemshukuru Raisi Dk Samia kwa kuanzisha kampeni hiyo kuwezesha jamii kupata huduma za msaada wa Kisheria.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria , Mkurungezi Msaidizi Huduma za Sheria kwa Umma Abdulrhaman Mshamu amesema lengo kuu la Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ni kulinda na kukuza upatikanaji wa haki kwa wote kupitia huduma ya Msaada wa Kisheria nchini.

Amesema kampeni imejikita katika kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi hususan katika masuala ya ukatili wa kijinsia, migogoro ya ardhi, mirathi, usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala na masuala yahusuyo haki za binadamu kwa ujumla.

“Utekelezaji wa kampeni hii ni utekelezaji wa sheria ya msaada wa kisheria namba 21 ya mwaka 2017 iliyotoa wajibu kwa serikali kuhakikisha inafikisha huduma za kisheria kwa wananchi wote” ameeleza

Mikoa 11, imefikiwa na Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia tangu kuanza mwaka 2023  na mwaka huu 2025 inaendelea katika mikoa sita ikiwemo mkoa wa Mtwara.

Habari Zifananazo

Back to top button