Msama apokea tuzo muandaaji bora matamasha ya injili

MKURUGENZI wa Msama Promotions, Alex Msama, amepokea tuzo ya heshima kutoka kwa Chama cha Muziki wa Injili Tanzania (CHAMUITA) kwa kutambuliwa kama muandaaji ora wa matamasha ya nyimbo za Injili kwa muda wote, kwa mchango wake mkubwa wa kuinua na kusapoti muziki huo.

Akizungumza na HabariLeo Dar es Salaam baada ya kupokea tuzo hiyo, alisema kuwa anashukuru kwa heshima aliyopewa na anaamini kuwa itampa motisha zaidi ya kuendeleza kazi ya kuinua muziki wa Injili.

Ameongeza kuwa amepitia safari ndefu ya maisha, ikiwemo kazi mbalimbali kama dereva na kubeba mizigo Kariakoo, lakini lengo lake kuu lilikuwa kusaidia waimbaji wa muziki wa Injili.

“Nashukuru kwa kutambua mchango wangu. Nitaendelea kusapoti muziki wa Injili na kuwasaidia wasanii wachanga, kama nilivyoshirikiana na waimbaji wakubwa kama Rose Muhando, Boniface Mwaitege, na Bahati Bukuku. Lengo langu ni kuhakikisha muziki huu unaendelea kukua na kuenea zaidi,” amesema Msama.

Aidha, amesisitiza kuwa tuzo hiyo si yake binafsi bali ni ya mashabiki wote na wapenzi wa muziki wa Injili nchini na nje ya nchi. Alitangaza kuwa Tamasha la Pasaka litafanyika kwa kishindo, huku akiahidi kuendelea kupigania muziki wa kumtukuza Mungu.

Msama pia amewataka wasanii wa Injili kujitofautisha na wasanii wa Bongo Fleva kwa kutoendeshwa na tamaa za vitu vya kidunia, bali kuzingatia utumishi wao kwa Mungu.

Kwa upande wake, Rais wa CHAMUITA, Ado Novemba amesema kuwa Msama ametambuliwa kwa mchango wake wa muda mrefu katika tasnia hiyo.

Miongoni mwa wasanii wengine waliopokea tuzo za heshima ni pamoja na Malkia wa nyimbo za Injili, Rose Muhando, na Cosmas Chidumule, aliyewahi kuwa mwimbaji wa dansi kabla ya kuokoka na kuanza kuimba muziki wa Injili.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button