MSD: Upatikanaji bidhaa za afya umeongezeka

DAR ES SALAAM: Bohari Kuu ya Dawa (MSD), imebainisha kuwa upatikanaji wa bidhaa za afya umeongezeka kutoka asilimia 51 mwezi Juni 2022 hadi kufikia asilimia 64 mwezi Juni mwaka 2023.

Kuongezeka huko kumechangiwa na serikali kutoa fedha za kutosha kwa ajili ya kufanya ununuzi wa dawa na vifaa tiba pamoja na usambazaji wake katika vituo vya afya.

Hayo yameelezwa jijini Dar es Salam na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mareva Tukai katika mkutano na waandishi wa habari na wahariri kuelezea taarifa ya utendaji, mafanikio na mwelekeo wa MSD.

Amesema katika kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba unazingatiwa, wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuzuia uagizwaji wa dawa kutoka nje ya nchi na badala yake wataendelea kusimamia uzalishaji dawa wa ndani kwa viwango vinavyohitajika.

Akizungumzia maboresho yaliyofanywa na MSD pamoja na mikakati iliyopo, Tukai amesema wameimarisha mifumo ya usimamizi kwenye ununuzi, kwa kushirikisha balozi zilizopo China, Algeria, Urusi na Korea Kusini kutafuta wadau wa uzalishaji na ununuzi, lakini pia wataendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuanzisha na kusimamia viwanda vya bidhaa za afya.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la wahariri (TEF), Deodatus Balile akizungumza kwa niaba ya wahariri ameishauri serikali kulipa deni wanalodaiwa na MSD, ili kuwezesha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa uharaka, pamoja na kupongeza ushirikiano uliopo kati ya MSD na sekta binafsi.

Habari Zifananazo

Back to top button