SERIKALI kupitia Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Dar es Salaam imesambaza vifaa tiba vya zaidi ya Sh milioni 930 kwa ajili ya vituo vya afya 24 vya halmshauri ya Wilaya ya Ulanga.
Akizungumza mkoani Morogoro Mbunge wa jimbo la Ulanga, Salim Hasham, amesema, wamepokea vifaa tiba hivyo na dawa za zaidi ya sh. milioni 900 kwa ajili ya vituo vya afya 23 vya halmashauri ya Wilaya ya Ulanga.
“Kishindo cha serikali ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan sekta ya afya ni kikikubwa, hivyo hatua ya kupokea vifaa tiba hivyo vya kisasa ni muendelezo wa maboresho sekta ya afya ambapo Ulanga na Mkoa wa Morogoro kwa ujumla ni wanufaika,”amesema Hasham.
Amesema, mbali na hatua hiyo wamepokea fedha sh. milioni 900 kwa ajili ya ukarabati wa hospitali ya wilaya, ambapo mazungumzo yanaendelea ili waweze kupatiwa eneo lingine litakalokidhi mahitaji ya wilaya hiyo, ambayo kwa sasa ni makubwa yakihusisha wawekezaji na wafanyabiashara wa madini ambao watapatiwa huduma.
Salim amesisitiza kuwa, wilaya hiyo ndani ya miaka mitatu imepata vituo vya afya viwili na zahanati 10 na cha kushangaza vipo vituo vya afya ambavyo havijamaliza ujenzi kikiwemo kituo cha afya cha Ruaha, lakini MSD imeshafikisha mahitaji yote muhimu vikiwemo vifaa tiba.
“Zamani vituo vya afya vilikuwa vinaisha na tunakaa kusubiri vifaa tiba zaidi ya mwaka, lakini kwa sasa vifaa tiba vinasubiri mmalize wafunge na wananchi wapate huduma kwa wakati mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, MSD mabadiliko ni makubwa sana MSD ya mama yetu Rais Samia sio ile tuliyokuwa tunainyooshea vidole kila wakati,”alisisitiza.
Naye Meneja wa MSD Kanda ya Dar es Salaam, Betie Kaema amesema, MSD kwa niaba ya serikali wanaahidi kutomuangusha Rais katika utekelezaji wa majukumu yake, hivyo upatikanaji wa uhakika wa dawa na vifaa tiba nchini utaendelea kuimarika zaidi, lengo likiwa ni kuboresha huduma za afya.
Amesema, ujio wa dawa na vifaa tiba hivyo vya zaidi ya sh. milioni 900 ni muendelezo wa maboresho hayo.
“Julai hadi Novemba tumehakikisha dawa na vifaa tiba vya sh. milioni 600 vinaletwa hapa na sasa tumekabidhi dawa na vifaa tiba vya zaidi ya sh. milioni 300, hivyo vituo vya afya 23 vya Ulanga watapata bidhaa za sh. milioni 900 ambazo zote zimekamilika na sasa vinasambazwa vituoni.
Alitaja baadhi ya vifaa tiba ambavyo wamepatiwa wananchi wa Ulanga kuwa ni kiti cha huduma ya meno, vitanda vya huduma ya uchunguzi, vitanda vya wodini vya wagonjwa, vifaa vya joto kwa ajili ya watoto njiti, vifaa vya kusaidia upumuaji, vifaa vya oxygen, vitanda vya upasuaji na Ultrasound mashine.
Vingine ni viti vya kubebea wagonja, vifaa vya kutundikia maji tiba, pasi ya hospitali, stendi ya pazia za kuzibia wagonja, mikebe ya vifaa vya kujifungulia, matoroli ya kutolea dawa, vitanda vya kujingulia na vinginevyo.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Alli Ramadhan, alisema kwa sasa hali ya huduma za afya wilayani humo imekuwa na maboresho makubwa kuanzia watumishi, dawa na vifaa tiba.
Amesema hali ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba ni asilimia 95 hadi 97 tofauti na awali ilikuwa ni asilimia 70 hadi 80, hali hiyo imepunguzaa malalamiko ya wananchi na kuwa na imani na watumishi wao.