Wakabidhiwa hatimiliki za mashamba
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi amegawa hati kwa wamiliki wa viwanja na mashamba 1,674 katika kijiji cha Msomera, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Waziri Ndejembi amesema ili kuharakisha mchakato wa umiliki wa ardhi kijijini humo, masharti ya utoaji yameboreshwa kwa kuondoa ‘ulazima’ wa mume na mke kuwa na Kitambulisho cha Taifa (NIDA).
Sasa mkuu wa kila kaya zikiwemo 139 zilizokutwa katika mpango wa kuhama kwa hiari kutoka Ngorongoro, mwenye NIDA, atapata hatimiliki, na masuala mengine yataachwa kwenye familia husika.
SOMA: Wakubali kuhamia Msomera
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Anthony Sanga amesema utoaji hati miliki ni endelevu ili wananchi wote wa Msomera wamiliki maeneo yaliyopangwa na kupimwa.
Mhandisi Sanga amesema awamu mbili za ugawaji hati miliki ambapo awamu ya kwanza zilitolewa hati 1,142 zikijumuisha nyumba 503, mashamba 500 na 139 za wenyeji waliokutwa kijijini humo na kwamba awamu ya pili zimetolewa hati 1,674 kwa ajili ya makazi na mashamba.
SOMA: Viwanja 10000 kupimwa wanaohamia Msomera
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batlida Buriani amesema serikali itaendelea kuboresha huduma kijijini humo, na kuwataka wakazi wake kuendelea kuziunga mkono jitihada hizo.
Amesema nia ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuboresha maisha ya Watanzania hilo linadhihirika katika ngazi zote za jamii na amemtunuku Mwenyekiti wa Msomera, Martine Paraketi Shilingi 100,000 kwa kueleza kwa ufasaha miradi ya maendeleo kijijini humo.