Mtaalamu: Hakuna malaria 1, 2 wala 3 wanapotosha!

DAR ES SALAAM; KAMA uliwahi kupima ugonjwa wa malaria na majibu ukaambiwa una malaria 1,2 au 3 tambua ulidanganywa na haipaswi kuwa hivyo.

Watu wengi wamekuwa wakikutana na majibu ya aina hiyo wanapoenda katika vituo vya afya kupima au hata maabara za kawaida mtaani, hali hiyo inawafanya kutumia dawa za kuua wadudu hao.

Ufafanuzi huo umetolewa na ofisa mteknolojia wa maabara kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Peter Torokaa alipoendesha mafunzo ya afya jijini Dar es Salaam Oktoba 26,  2023.

Ofisa huyo alifafanua baadhi ya wataalamu wa maabara wa vituo vya kutolea huduma za afya wamekuwa wakipotosha kwenye uchunguzi wa malaria, hivyo kusababisha kutoa majibu yasiyokuwa sahihi.

Torokaa alieleza kwenye tone moja la damu kuna uwezekano wa kuwa na seli nyeupe za damu zaidi ya 5000, mtaalamu wa Maabara anatakiwa kuanza kuhesabu seli nyeupe za damu pindi anapoona kimelea wa malaria.  Hivyo Kuna uwezekano wa kuuona vimelea 1000 kwenye kila seli 1 nyeupe ya damu.

Kwanini wataalamu wa maabara vituo vya afya wamekuwa wakitoa majibu ya watu kuwa na malaria 1, 2 au 3?

Mtaalamu Torokaa anasema baadhi ya wataalamu hao wamekuwa wakianza kuhesabu seli nyeupe za damu pindi tu wanapomuona kimelea.

Wanatakiwa kufanyaje sasa ili kutoa majibu sahihi? Torokaa anasema wanachotakiwa kufanya ni kuangalia katika seli nyeupe 200 za damu wameona wadudu wangapi?.

“Baadhi ya maabara na famasi vimekuwa vikijiendesha kibiashara hivyo ni sababu mojawapo, mbili baadhi ya wagonjwa huwa hawaridhishwi na majibu ya kuambiwa kutokuwa na ugonjwa wowote,” anasema Torokaa.

Anasema kwa kufanya hivyo, watalamu hao wamekuwa wakikosea na kwenda kinyume na taratibu za miongozo ya utoaji majibu ya malaria, amesema Peter Torokaa.

Amesema Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais Tamisemi na waratibu wa masuala ya afya ngazi ya halmashauri na Mikoa wamekuwa wakifanya ukaguzi wa aina hiyo ya wataalamu na wasimamizi wa maabara hizo ili kuwachukulia hatua za kisheria na kinidhamu.

Habari Zifananazo

Back to top button