Tuache chokochoko tudumishe amani

MUFTI na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir, amewataka Watanzania kuendelea kudumisha uzalendo na kuitunza tunu ya amani iliyopo nchini, akisisitiza kwamba choko choko za kisiasa na mitazamo yenye kugawa jamii zinaweza kuhatarisha umoja wa kitaifa.

Akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Njombe, Sheikh Zubeir alisema kuhubiri amani ni msingi wa mafundisho ya Uislamu na ni msimamo wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), ambalo limekuwa mstari wa mbele katika kuhimiza uadilifu, upendo na heshima miongoni mwa watu wote bila kujali dini au itikadi za kisiasa.

“Amani ndiyo nguzo ya maendeleo. Kila Mtanzania ana wajibu wa kuilinda ili ibaki kuwa urithi wa vizazi vijavyo,” alisema Mufti Zubeir. Alisisitiza kuwa BAKWATA si taasisi ya kisiasa wala kibaraka wa serikali, bali ni chombo cha kidini kinachojitegemea, kinachoendesha shughuli zake kwa misingi ya maadili mema na ustawi wa kijamii.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, aliliomba baraza hilo kuanzisha vitega uchumi vitakavyokiwezesha kujitegemea kiuchumi, ikiwemo kumiliki ardhi na miradi ya uzalishaji mali. “Ni wakati sasa taasisi za dini ziwekeze kwenye miradi yenye tija kama elimu, afya na huduma za kijamii, ili kusaidia kupunguza utegemezi na kuboresha maisha ya waumini,” alisema Mtaka.

Mtaka aliongeza kuwa taasisi za dini ni wadau muhimu wa maendeleo na zinapaswa kutumia nafasi hiyo kushirikiana na serikali katika kujenga jamii yenye amani, umoja na maendeleo endelevu. SOMA: Nchimbi asema Bandari Kwala ni mageuzi kiuchumi

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button