Muhalila Cup yawapa vijana wenye vipaji Tabasamu
KAGERA; Wadau wa michezo mkoani Kagera wametakiwa kujitokeza viwanjani kushuhudia vipaji vinavyoendelea kuoneshwa katika Ligi ya Muhalila Cup ambayo ipo katika mzunguko wa pili ndani ya viwanja vya Kagoma ambapo timu 16 zinatunishiana misuli kuwania kitita cha Sh milioni mbili.
Mratibu wa Mashindano hayo ,Mwalimu Adrofu Kahinga anasema kuwa mashindano hayo yanaendelea vizuri na vijana wanaonyesha vipaji.
“Vijana wanavipaji vingi ni vizuri wadau wa michezo ambao wanaendesha michezo na ligi mbalimbali kuja uwanjani kushuhudia mashindano hayo ,kwa sasa tuko mzunguko wa pili na ukiisha tunaingia mzunguko wa mwisho wa kuitafuta robo Fainiali ,kwa miaka tisa mfululizo wa ligi hii Kuna mengi sana ya kujifunza ,tutumie mashindano hayo kuwapa vijana hamasa”anasema Kahinga.
Katibu wa Chama cha mpira wa Miguu Wilaya ya Muleba (MDFA), Hosea Shedrack anasema kuwa wadau mbalimbali wanaoendesha ligi za vijijini wataendelea kupata vibali vya kuendesha ligi hizo ili kuwawezesha vijana kuonyesha vipaji vyao na kushiriki hatua mbalimbali za mashindano ya ligi kuu na ligi nyingine za taifa.
Anasema uwepo wa mashindano ya Muhalila cup kwa miaka tisa mfululizo yameitangaza Wilaya ya Muleba na mkoa wa Kagera kwa ujumla na baadhi ya vijana waliopitia Iigi hiyo wanacheza katika ligi kuu ya Tanzania.
Alitoa wito kwa vijana waliopata Fursa ya kushiriki ligi hiyo kuhakikisha wanaonyesha uwezo mzuri maarifa ya michezo uwajibikaji katika timu zao na nidhamu ili kujiandalia nafasi nzuri ya juu zaidi.
Mchezaji wa zamani wa Timu ya Costal unioni ,Salawa Mpunda amepongeza mwitikio wa vijana na hamasa ya jamii jinsi wanavyojitoa kwa wingi kuangalia timu zao huku akisisitiza kuwa wadau wanaotaka kuangalia vipaji wavifuate uwanjani.
Fainali za mashindano hayo zitafanyika katika uwanja wa shule ya Sekondari Kagoma Desemba 31, 2023.