Muhas yataja mafanikio yake

CHUO Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) kimesema kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Uchumi (HEET) kimefanikiwa kupitia mitaala na kuboresha mitaala 82 ya shahada ya uzamili na programu mitaala 23 ya programu mpya.

Hata hivyo Muhas imefanikiwa katika upatikanaji wa mtandao wa mawasiliano ‘internet’ na matumizi ya mifumo ya kidigitali katika Kampasi ya Muhimbili.

Advertisement

Akizungumza katika mahafali ya 18 ya chuo hicho yaliyofanyika leo chuoni hapo Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Dk Rehema Horera amesema sambamba na mafanikio hayo, pia Muhas imefanikiwa kupeleka wanataaluma 33 katika mafunzo ya uzamili na shahada za uzamiivu ndani ya nje ya nchi kuwajengea uwezo wa kufundisha.

“Kitengo cha kuzalisha mapato na mpango wa biashara umeandaliwa na kupitishwa  na baraza la chuo kwa ajili ya utekelezaji,” amesema Dk Horera.

Akizungumza chuoni hapo, Dk Horera amesema miongozi miwili ya jinsia imetengenezwa na kuidhinishwa na baraza la chuo ambayo ni Sera ya Kuzuia na Kupambana na Unyanyasaji wa Kijinsia, na Sera ya Ujumuishaji wa Jinsia.

Akizungumzia mahafali hayo, Makamu Mkuu wa Muhas, Profesa, Apolinary Kamuhabwa amesema jumla ya wahitimu ni 1,309 kati ya hao, 461 ni wahitimu wa kike ambao ni asilimia 35 ya wahitimu wote, aidha amesema lengo la chuo ni kuwa na asilimia sawa kwa kuwawezesha wanafunzi wa kike kujiunga na program mbalimbali.

Amesema wahitimu 199 wametunukiwa stashahada na stashahada ya juu katika fani mbalimbali za afya na sayansi shirikishi. Pia wahitimu 708 wamepatiwa shahada ya kwanza na wengine 441  shahada ya uzamili, wengine 33 wametunukiwa digrii za uzamili na bobezi, aidha wengine 8 wametunukiwa digrii ya uzamivu ya udaktari wa falsafa.

“Aidha katika mahafali haya tunao wahitimu 2 wa program mpya ya shahada ya uzamili na ubobezi kwenye uchunguzi wa magonjwa ya wanawake kwa kiradiojia ambayo imeanza kutoa wahitimu mwaka huu wa 2024,” amesema Kamuhabwa.

Akizungumza kwa niaba ya wahitimu wenzake, mhitimu Satrumin Arbogast wa digrii ya kwanza, amesema amewataka wanafunzi wenzake kuwa wanapaswa kutumia changamoto kama sehemu ya kukua.

“Tuwe na ujasili na uvumilivu, tukijua kwamba kikwazo kinaweza kutupelekea kwenye mafanikio,” amesema.

Katunzi Mutalemwa mwanafunzi wa digrii ya uzamili amewataka wahitimu wenzake kutumia ujuzi na umahiri waliopata wakati wa masomo ili kutoa huduma nzuri na bora.

“Naomba tujipe changamoto ya kuwa na ndoto kubwa zaidi, kwani hapa ni mwanzo wa safari ya umahiri wa juu wa afya, hivyo nawahimiza wahitimu wenzangu tusiishie hapa,” amesema.