Muktadha wa kitaifa kwa aliyepewa ujauzito kwa kubakwa

Karibu katika makala inayochambua suala tata la utoaji mimba kwa wanawake waliobakwa, hususa wale wenye ulemavu, kwa muktadha wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Pia tutaangazia mtazamo wa kimataifa ili kutoa mwanga mpana kuhusu haki na ulinzi wa waathirika hawa. Utoaji mimba kwa aliyebakwa: muktadha wa kisheria na kimaadili

Utoaji mimba ni suala lenye mjadala mpana duniani, lakini linapohusisha wanawake waliobakwa — hususan wenye ulemavu — hoja huwa nzito zaidi. Swali linabaki: Je, mwanamke aliyebakwa ana haki ya kutoa mimba?

Sheria ya Utoaji mimba kwa aliyebakwa Tanzania, pamoja na nchi jirani kama Kenya na Uganda, utoaji mimba ni haramu isipokuwa kwa madhumuni ya kuokoa maisha au afya ya mama.

Kwa mujibu wa Kanuni ya Adhabu (Penal Code) ya Tanzania, Kifungu cha 230–234, utoaji mimba unaruhusiwa pale tu ambapo afya ya mwathirika imo hatarini.

Hata hivyo, sheria haijafafanua wazi iwapo ubakaji pekee unaweza kuwa msingi halali wa utoaji mimba, ila madaktari wanaweza kuingilia iwapo mimba inaathiri afya ya mwathirika — kimwili au kisaikolojia.

Licha ya Tanzania kuridhia Mkataba wa Maputo zaidi ya miaka 15 iliyopita, utekelezaji wa baadhi ya vipengele muhimu vya mkataba huo, hasa Ibara ya 14 inayohusu haki ya afya ya uzazi kwa wanawake, umeendelea kuwa changamoto kutokana na vikwazo vya kisheria, kijamii na kiimani.

Mkataba wa Maputo, ambao ni nyongeza ya Mkataba wa Afrika kuhusu Haki za wanawake, unasisitiza haki ya wanawake kupata huduma salama za afya ya uzazi, ikiwemo huduma ya utoaji mimba katika mazingira yasiyosahihi kama vile, ubakaji, mimba za maharimu na shambulio la ngono.

Hata hivyo, sheria za Tanzania kupitia Kanuni ya Adhabu (Penal Code) kifungu cha 150, 152, 153 na 230, bado zinakataza utoaji wa mimba, isipokuwa pale tu inapolenga kuokoa maisha ya mama. Hali hii inaonekana kupingana na masharti ya Ibara ya 14 ya Mkataba wa Maputo.

Habari leo, ilipata nafasi ya kuzungumza na mwanasheria Clay Shina, ambaye pia ni mdau wa haki za wanawake kutoka taasisi ya kijamii inayojihusisha na afya ya uzazi, alisema kuwa Tanzania haijafanya marekebisho ya sheria zake za ndani ili kuendana na matakwa ya Mkataba wa Maputo.

“Tunaposema Tanzania haijatekeleza mkataba huu, tunamaanisha kuwa bado haijabadilisha sheria ili kuwezesha upatikanaji wa huduma salama za afya ya uzazi kwa wanawake waliopo kwenye mazingira hatarishi,” anasema.

Kwa mujibu wake, changamoto kubwa inayozuia utekelezaji wa ibara hiyo ni mitazamo ya kijamii na imani za kidini ambazo haziruhusu utoaji wa mimba, hata katika hali za dharura.

“Katika dini ya Kiislamu hakuna shehe mwanamke msikitini, wala padri mwanamke kanisani. Lakini wanawake wanaruhusiwa kuongoza maeneo mengine. Hii inaonesha kuwa tunaweza kutafuta njia ya kati ili haki za wanawake zitekelezwe bila kuvunja misingi ya dini,” aliongeza.

Aidha, alieleza kuwa nchi kama Rwanda na Afrika Kusini tayari zimefanya mabadiliko ya kisheria kuruhusu utoaji wa mimba katika mazingira yaliyoainishwa na Maputo Protocol.

Rwanda, kwa mfano, inahitaji mwanamke kupata vyeti kutoka kwa madaktari wawili tofauti pamoja na idhini ya mahakama kabla ya kuruhusiwa kutoa mimba. Afrika Kusini imekwenda mbali zaidi kwa kuruhusu huduma hiyo hata kwa sababu za kiuchumi na kijamii.

“Tanzania inaweza kujifunza kutoka kwa nchi hizo bila kuiga kila kitu. Tunaweza kuchukua kilicho bora kutoka Rwanda na Afrika Kusini na kukiweka katika mazingira ya nchi yetu,” anasema.

Alisema kuwa baadhi ya wanawake wana matatizo ya afya ya akili na hushindwa kulea watoto waliowazalia mitaani, huku wengine wakijifungua kutokana na ubakaji au mimba zisizotarajiwa bila kupata msaada wa kisheria wala wa kiafya.

Alitaja kampeni ya “Muache Asome” kuwa miongoni mwa mikakati inayoweza kusaidia wasichana waliopata mimba kurudi shule, lakini akasisitiza kuwa bila mabadiliko ya sheria na uhamasishaji wa jamii, mafanikio yatakuwa haba.

“Sheria inaweza kupitishwa, lakini ikashindwa kutekelezwa kutokana na hofu, imani potofu au ukosefu wa elimu kwa jamii,” anasema.

Amezitaka taasisi husika zikiwemo Wizara ya Katiba na Sheria, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Tume ya Marekebisho ya Sheria na Wizara ya Afya kushirikiana kuhakikisha sheria zinahuishwa na utekelezaji wake unaenda sambamba na mkataba huo wa kimataifa.

Kwa mujibu wa Clay utafiti uliofanywa na taasisi ya Guttmacher Institute, World Health Organization (WHO), na pia African Union kupitia tathmini ya utekelezaji wa Maputo Protocol kuhusu afya ya uzazi barani Afrika umeonesha kuwa utekelezaji wa Maputo Protocol unaweza kupunguza zaidi ya asilimia 13 ya vifo vinavyotokana na mimba hatarishi au zisizotarajiwa.

Simulizi ya Maumivu: Kisa cha Mariam Peter

Mariam Peter, msichana mwanafunzi na mwenye ulemavu wa kusikia kutoka mkoani Pwani, alibakwa akiwa na miaka 14 na baadaye kugundulika kuwa mjamzito.

Akiwa anaendelea na masomo ilimpasa kuacha shule na kuanza kulea mimba.

Kutokana na hali yake, alishindwa kueleza kilichomtokea kwa ufasaha na sauti yake haikusikika.

Alipojifungua, alibeba mzigo wa ulezi na majeraha ya kisaikolojia peke yake.

Hana msaada na nyumbani alipokuwa akiishi ni kwashangazi yake amemfukuza na kumwacha akiwa anatapatapa mitaani huku akiwa mjamzito na pia ni mlemavu.

Mariam anashinda na kulala kwenye mabanda akitafuta msaada wa kuishi kula na kumtunza mwanae akiwa Hana msaada wa mtu yoyote wala hamjui baba wa mtoto huyo.

Leo hii, Mariam ni mama anayeshinda mitaani Hana pakwenye ndoto zake zilikatishwa kwa kubakwa anayeishi na mtoto wake akilelewa bila kumfahamu baba yake.

Jamii Inaponyamaza Katika mazingira ambapo watu wenye ulemavu wanahitaji ulinzi na huruma zaidi, bado wanaachwa katika kivuli cha ukatili.

Unyanyapaa, dharau, na kimya cha kijamii vinazidisha mateso ya waathirika. Wengi huonekana kama wasio na thamani au wanaostahili yaliyowapata — dhana ambayo ni dhalimu na hatari.

Kwa upande wake, Mkufunzi wa Kitaifa wa Masuala ya Afya ya Uzazi, Mgeni Kisesa, anasema endapo serikali itapitisha sheria ya kuruhusu utoaji wa mimba zisizotarajiwa, itawasaidia wanawake wanaopata mimba kutokana na ukatili wa kijinsia kama kubakwa au kulazimishwa.

“Kama sheria itaruhusu, tutaweza kuwasaidia wanawake wengi kuepukana na janga hili kwani kwa sasa, nchi yetu hairuhusu utoaji wa mimba isipokuwa ikiwa maisha ya mama yako hatarini,” anasema Kisesa.

Kisesa alieleza kuwa sheria hiyo pia itaokoa maisha ya wanawake wengi kwa kupunguza utoaji wa mimba usio salama.

“Mimba hizi zisizotarajiwa husababisha utoaji wa mimba usio salama, ambao una athari nyingi ikiwemo vifo vya asilimia 10 hadi 16 ya wanawake,” aliongeza.

Alisisitiza umuhimu wa wanawake waliobakwa kufika kituo cha afya ndani ya saa 72 ili kupata huduma stahiki kama vile dawa za kuzuia mimba na kuzuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

“Kuna changamoto ya watu kuchelewa kufika kituo cha afya, hivyo kukosa huduma za kuzuia mimba,” alisema.

Aidha, alieleza kuwa mwanamke aliyepata mimba isiyotarajiwa hawezi kwa sasa kupata huduma ya kutoa mimba kwa mujibu wa sheria, isipokuwa pale inapothibitishwa kuwa mimba inahatarisha maisha yake.

“Tunawashauri kuhusu athari za utoaji wa mimba usio salama, na kuwashauri kubaki na mimba hiyo. Hata hivyo, tunafahamu kuwa dunia ya sasa imejaa njia nyingi za kutoa mimba, na hivyo huwaambia warudi hospitalini endapo watapata matatizo,” anasisitiza.

Kisesa alihitimisha kwa kusema kuwa “kupitishwa kwa sheria ya kuruhusu utoaji wa mimba kwa mazingira maalum kutasaidia kuokoa maisha ya wanawake wengi walioko hatarini.

Haki na Ulinzi wa Kisheria Ripoti hii inaonesha takwimu na hali ya makosa ya ubakaji yaliyoripotiwa katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2024.Imetolewa na Kamishna wa Operesheni na MafunzoJeshi la Polisi Tanzania Tarehe: 05 Mei 2025

Lengo ni kutoa tathmini ya mwenendo wa uhalifu huu na kuchochea mikakati ya kupambana nao.

Takwimu za ujumla Katika kipindi cha mwaka 2024, jumla ya makosa 6,735 ya ubakaji yaliripotiwa nchini kote. Hii ni ongezeko la asilimia 8.2% ikilinganishwa na makosa 6,225 yaliyoripotiwa mwaka 2023.

Maneno yalioathirika zaidi Mikoa iliyoripoti idadi kubwa ya matukio ni: Dar es Salaam – 1,208 kesi, Mwanza – 864 kesi, Mbeya – 712 kesi, Arusha – 630 kesi, Dodoma – 589 kesi

Wanaoathirika zaidi ni watoto wa kike chini ya umri wa miaka 18: 4,921, Wanawake watu wazima: 1,621, Watu wenye ulemavu: 193

hatua zilizochukuliwa Kesi zilizofikishwa mahakamani: 4,352 Watuhumiwa waliotiwa mbaroni: 5,108 , Kesi zilizoamuliwa: 1,287 (asilimia 29.6% ya zilizofikishwa mahakamani), Hukumu za hatia: 847, Hukumu za kutokuwa na hatia: 440

Changamoto zilizoibuka changamoto zilizoibuka Waathirika wengi kutotoa taarifa kwa wakati,

Ucheleweshaji wa ushahidi wa kitabibu, Hofu ya unyanyapaa kwa waathirika, Baadhi ya kesi kumalizwa kifamilia bila kufikishwa mahakamani

Kwa mujibu wa ripoti ya jeshi la Polisi ya mwaka 2024/imetolewa Mei 2025 iliyotolewa na Kamishna mkuu, linasema kuzuia vitendo hivyo ni Kuimarisha elimu kwa jamii juu ya madhara ya ubakaji, Kuweka vituo rafiki kwa waathirika, Kufanya uchunguzi wa haraka na wa kitaalamu, Kuweka sheria kali zaidi kwa wahalifu wa makosa ya ubakaji

Jeshi la Polisi linaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha makosa ya ubakaji yanapungua na waathirika wanapata haki stahiki. Ulinzi wa watoto na wanawake ni jukumu la kila Mtanzania.

Familia nyingi hukataa kutoa ushirikiano kwa hofu ya aibu au mahusiano ya kifamilia.
Sheria inahitaji kufanyiwa marekebisho ili kuhakikisha ulinzi wa haki za watu wenye waliobakwa hasa ulemavu. Pendekezo:

Kuwepo na watafsiri wa lugha ya alama katika hatua zote za kisheria.
Kuweka mfuko wa msaada maalum kwa waathirika wanaobeba ujauzito kwa kubakwa.Tuwaone, Tuwasikie, Tuwalinde

Msichana, mwanamke na mwenye ulemavu anapobakwa na kuachiwa na mimba, jamii nzima ina jukumu la kuwajibika.Hatuwezi tena kunyamaza.

Hii siyo vita ya mtu mmoja, bali ni vita ya utu, haki, na heshima ya kila binadamu.Haki si zawadi, ni wajibu wa jamii kuilinda. Tunapaswa kutenda haki sasa

Tunapochagua kunyamaza wakati wanawake na wasichana na wanaobwakwa hasa walemavu wanateseka kwa ukatili, tunakuwa washirika wa dhuluma.

Ni wakati wa kuamka:Tuwashinikize wabunge kupitisha sheria itakayomsaidia msichana au mwanamke aliyebakwa na kupata mimba ili kufikia malengo yake.

Tuimarishe elimu na uelewa katika jamii kuhusu haki za watu, waliobakwa.Tuunde mifumo rafiki inayowalinda na kuwapa msaada wa kweli watu waliobakwa.
Usikivu wetu uwe mlinzi wao. Sauti zetu ziwe ngao yao. Hatua zetu ziwe tumaini lao.

Lakini je, heshima ya familia ni muhimu kuliko haki ya aliyebakwa hasa kwa mlemavu?Wapi Msaada wa Kisaikolojia na Kijamii?Waathirika wengi huachwa bila ushauri nasaha, msaada wa kifedha, au hata neno la faraja.

Wito kwa Wabunge na Wana Sheria Tanzania kuridhia Mkataba wa Maputo zaidi ya miaka 15 iliyopita, utekelezaji wa baadhi ya vipengele muhimu vya mkataba huo, hasa Ibara ya 14 inayohusu haki ya afya ya uzazi kwa wanawake, umeendelea kuwa changamoto kutokana na vikwazo vya kisheria, kijamii na kiimani.

Mkataba wa Maputo, ambao ni nyongeza ya Mkataba wa Afrika kuhusu Haki za wanawake, unasisitiza haki ya wanawake kupata huduma salama za afya ya uzazi, ikiwemo huduma ya utoaji mimba katika mazingira yasiyosahihi kama vile, ubakaji, mimba za maharimu na shambulio la ngono

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button