Muziki si bangi, ni mapambano ya maisha

LAGOS, NIGERIA : MSANII nguli wa Afrobeat kutoka kundi la P-Square, Paul Okoye maarufu kama Rudeboy au King Rudy, ametoa onyo kali kwa wasanii wachanga kuhusu matumizi mabaya ya bangi na sigara kwenye tasnia ya muziki.
Kupitia Instagram Story yake, Rudeboy alionyesha kutoridhishwa na tabia ya baadhi ya vijana kurekodi video wakivuta bangi kwa lengo la kuonekana “cool” au maarufu kwenye mitandao. “Wimbo hata haujaanza sekunde 20, tayari mnaanza kuvuta bangi kwa ajili ya kamera? Mnaonekana wagonjwa!” aliandika kwa ukali.
Amesisitiza kuwa baadhi ya wasanii hutumia fedha nyingi kununua bangi huku wakishindwa hata kula vizuri au kujali afya yao ya mwili na akili. Kwa mujibu wa Rudeboy, tabia ya kuvuta bangi siyo alama ya ubunifu wala “swag”, bali ni presha inayotokana na kutaka umaarufu wa haraka. “Swag sio sigara au bangi. Kitu cha maana ni akili timamu na afya njema.”
Ametoa wito kwa wasanii wapya kuzingatia afya zao kama msingi wa mafanikio ya muda mrefu katika muziki, akisema kuwa tasnia hiyo ni mapambano ya maisha, si maigizo ya mitandaoni. SOMA: Wanafunzi wapewa somo udhibiti dawa za kulevya
Kauli ya Rudeboy imeibua mjadala mkubwa kuhusu athari za mitindo ya maisha isiyo na mwelekeo sahihi miongoni mwa wasanii chipukizi, hasa wanaojitahidi kujitambulisha katika ulimwengu wa burudani unaoshindana kwa kasi.



