Mwanafunzi afa kwa kuonja kemikali maabara

Aacha ujumbe mzito

KATAVI: Mwanafunzi mmoja wa shule ya sekondari St. Mary’s iliyopo Manispaa ya Mpanda Luis Emmanuel (17) amefariki baada ya kunywa kemikali inayodhaniwa kuwa ni ethanol katika maabara ya shule hiyo akiwa na wanafunzi wengine wawili.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi SACP Kaster Ngonyani amesema tukio hilo limetokea mnamo Mei 25, 2024 majira ya saa 5 asubuhi ambapo amewataja wanafunzi wengine ni Evangelist Deodatus (20) na Anastazia Zakayo (17) wote kidato cha nne.

Amesema wanafunzi hao watatu walikuwa wakifanya usafi katika maabara ya kujifunzia masomo ya sayansi kwa vitendo iliyopo shuleni hapo huku wakisimamiwa na mwalimu John Mtafya ambaye baadae alitoka nje kuendelea na shughuli nyingine za kimasomo na kuwaacha wanafunzi hao wakiendelea na usafi, ndipo walipoingia katika chumba cha kuhifadhia kemikali ambapo walichukua kemikali hiyo ya ethanol na kisha kuinywa.

“Baada ya kumaliza usafi mwalimu alirudi nakufunga maabara ile na wanafunzi wale walielekea darasani kuendelea na masomo” amesema SACP Ngonyani

Baada ya muda mfupi mmoja wa wanafunzi hao alianza kulalamika maumivu ya tumbo, ambapo alipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Mpanda kwa matibabu na huko alieleza kuwa yeye  pamoja na wenzake wawili wamekunywa kemikali, ndipo wote kwa pamoja walifikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi kwa matibabu.

Wakati wakiendelea na matibabu mwanafunzi Luis Emmanuel alipewa rufaa kwenda kupata matibabu zaidi katika Hospitali ya Rufaa Bugando Mwanza na alifariki dunia Mei 28, 2024.

Hata hivyo mwanafunzi Evangelist Deodatus anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi na Anastazia Zakayo hali yake ni njema na anaendelea na masomo.

Akizungumza kwa masikitiko Mashaka Nkana ambaye ni Baba mzazi wa Marehemu Luis Emmanuel amesema baada ya kupigiwa simu na uongozi wa shule alimfuata mtoto wake na kumpeleka hospitali kwa ajili ya matibabu ambapo alipimwa malaria, typhoid, UTI na sukari na kuambiwa kuwa hakukutwa na ugonjwa isipokuwa typhoid afuate majibu kesho yake.

“Wakati wote mtoto wangu alikuwa akilalamika kuwa na maumivu ya tumbo na macho anaona giza na alikuwa anataka kutapika lakini anashindwa..,alitapika kidogo mara moja” amesema Nkana

HabariLEO ilipomuuliza baba huyo kuhusu kauli ya mwisho ya marehemu alijibu kuwa “alizungumza mambo mawili, kuna moja alikwenda kuoga nikamfuata nikamkuta ameinama hakuoga baada ya kumuuliza akasema ‘nasikitika baba yangu unapoteza sana hela juu yangu’ baada ya hapo nikamjibu kuwa wewe ni mtoto wangu nina wajibu wa kufanya hivi, hivyo usijali kuhusu hela ninachojali ni uhai wako”amesema

Ameongeza kuwa baada ya hapo marehemu hakuongea neno lingine hivyo akamshika mkono na kuingia ndani na mara ya mwisho wakati wakiwa hospitali alisema kuwa ‘Baba nimechoka’.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mpanda ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya hiyo, Jamila Yusuf alipofika kwenye msiba huo kutoa salamu za pole amesema kama Serikali wameunda kamati ya uchunguzi ili kuchunguza juu ya tukio hilo lengo ni kuhakikisha matukio mengine kama hayo hayatokei kwenye shule nyingine.

Habari Zifananazo

Back to top button