Mwarobaini mikataba mibovu yachemka

DAR ES SALAAM: WIZARA ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) imeendesha mafunzo kwa wasuluhishi kwa njia mbadala ili kuwajengea uwezo katika uandishi wa vipengele vya utatuzi wa migogoro ndani ya mikataba pia kupunguza uandishi wa mikataba mibovu.

Mafunzo hayo, yanayofanyika kwa awamu mbili kuanzia Septemba 04 hadi 06 kisha kuendelea tena Septemba 09 hadi 11 mwaka huu jijini Dar es Salaam. Takribani wasuluhishi 50 wanatarajiwa kunufaika na mafunzo haya.

Akielezea kuhusu mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Usuluhishi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Felix Chakila amesema yataongeza ufanisi na tija kwa wataalam hawa hususani katika kutatua migogoro kwa njia mbadala.

“Wataalam hawa wamejengewa uwezo katika maeneo ya kutatua mgogoro kupitia majadiliano na usuluhishi na maadili ya kazi,” amesema mkurugenzi huyo.

Mafunzo hayo yametolewa na Wakufunzi wa ndani na nje ya nchi, wakiwemo Wakili Mkuu wa Serikali Mstaafu na Naibu Makamu Mkuu wa Taasisi ya Uanasheria kwa Vitendo, Dk. Clement Mashamba,  Rais wa Taasisi ya Uamuzi Tanzania na Mwanajopo wa Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji kutoka Tanzania, Madeline Kimei sambamba na Mwanasheria Mwandamizi na Msuluhishi kutoka Kosovo, Ahmet Kasumi.

Wasuluhishi katika mafunzo ya kujengewa uwezo

 

Umuhimu wa taaluma hii ya usluhishi ni kutatua migogoro, kuishauri serikali katika mikataba pia kuokoa fedha. Ukirejea, Julai 08 mwaka huu Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi  kilifanikiwa kuokoa zaidi ya Sh bilioni tano kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu, baada ya kusuluhisha kesi 42 kati ya mashauri 140.

SOMA: Bil 5/- zaokolewa usuluhishi Mahakama Kuu miezi mitatu

Akiwa jijini Dar es Salaam, Naibu Msajili Augustina Mmbando alisema mahakama hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Juni 30, mwaka huu wamepokea mashauri 152 na kati ya hayo yaliyofaulu kwenye usuluhishi ni 42 huku mashauri 98 yakiendelea kusikilizwa.

Mmbando alisema usuluhishi umesaidia kuokoa Sh bilioni tano na kwamba wanatarajia kuokoa zaidi ya Sh bilioni 10 kwa sababu endapo mashauri hayo yangeenda kusikilizwa katika mahakama za kawaida, yangechukua muda mrefu na gharama za uendeshaji wa kesi zingeongezeka.

“Fedha hizi zinaokolewa kwa namna hii, kama kuna mtu anakudai shilingi milioni 500 mnapokuja kusuluhisha mdaiwa anaweza kukuomba akulipe milioni 200 na ukikubali basi fedha iliyobaki inakuwa faida kwa sababu mngeenda katika mahakama za kawaida ni lazima ungelipa fedha yote,” alifafanua.

Habari Zifananazo

Back to top button