Mwekezaji alizeti alia na changamoto ya usafarishaji
MWEKEZAJI wa Kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti cha Singida Fresh Oil Mill amemlalamikia Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo uwepo wa vizuizi vingi barabarani wakati wa kusafirisha bidhaa za mazao ya kilimo katika barabara kuu kwa kutozwa tozo katika kila wilaya utakayopita na bidhaa hizo.
Akizungumza mbele ya Chongolo leo katika ziara yake kiwandani hapo wilayani Singida,aliootembelea kukagua uzalishaji wa alizeti,Msimamizi wa kiwanda hicho,Jamal Juma amesema wakati mwingine hulipa tozo ya bidhaa hiyo hiyo hata mara tatu.
“Changamoto kubwa bidhaa za mazao ya kilimo kama mashudu ya alizeti tumepata soko Kenya,lakini kuyasafirisha utalipia tozo Singida,Oldonyosambu na Longido kwa bidhaa hiyo hiyo,tunaishauri serikali tulipie tozo mara moja eneo bidhaa inakozalishwa,”amesema Juma.
Akizungumzia hilo Chongolo amesema ni wakati sasa wa halmashauri kutafuta vyanzo vya mapato badala ya kusiburi kutoza tozo za kudandia.