‘Mwendokasi’ ukiimarika utachochea uchumi

MWAKA 1968 nilifika Dar es Salaam. Wakati huo, wakazi wa mji huo hawakuwa wengi kama ilivyo sasa. Wakati huo usafiri jijini humo ulikuwa unatolewa na Dar-es-Salaam Motor Transport (DMT).

Taarifa zilizopo zinaonesha kuwa, usafirishaji abiria kupitia DMT ulianzishwa 1947 ili wakazi Dar es Salaam wapate usafiri wa uhakika na salama kuwahi katika maeneo ya kazi na uzalishaji mali na kwingine.

DMT ilikuwa ikisimamiwa na kampuni ya Waingereza iliyoitwa British Holding Cooperation United iliyoendesha shughuli za DMT kwa kufuata utaratibu uliozingatia ratiba kwa kujali muda.

Advertisement

Kupitia utaratibu huo abiria walijua basi litapita kituoni muda gani hivyo kuwahi kufika na kupata usafiri kwa wakati husika. Mwaka 1967, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alitangazia sera ya Ujamaa na Kujitegemea kama msingi
wa Watanzania kujiletea maendeleo kwa kutumia rasilimali watu, ardhi (yakiwemo madini na maliasili) siasa safi na uongozi bora.

Msisitizo uliwekwa kwa Watanzania kufanya kazi kwa bidii na kuzalisha mali kwa kutumia nguvukazi vizuri na kuzingatia weledi, akili na maarifa. Kupitia sera hiyo kuliwekwa msisitizo kwa watu kutokuwa ‘kupe’ bali kila mwenye uwezo wa kufanya kazi, afanye kazi.

Ikawekwa wazi kabisa kuwa, ‘ubepari ni unyama, ujamaa ni utu.’ Haya yalilenga kujenga jamii na taifa lenye watanzania wenye moyo wa kufanya kazi kujiletea maendeleo. Wakati huo, huduma za usafiri kwa wakazi wa Dar es
Salaam zilikuwa zikitolewa na DMT.

Ingawa changamoto zilikuwepo, si kuona wasafiri wakirundika kituoni kwa muda mrefu kusubiri usafiri. Ndiyo maana kwa mtazamo wangu, huduma za usafiri wa ‘mwendokasi’ zikiboreshwa zitakuwa bora na zenye tija zaidi.

Hata hivyo, mwaka 1970 baada ya serikali kuazimia kuuweka uchumi mikononi mwa umma (badala ya kumilikiwa na wachache) kukawepo sera ya ‘kutaifisha’ baadhi ya maeneo ya kiuchumi likiwemo la usafirishaji. Tangu wakati huo kampuni ya DMT (ikiwa ni kampuni binafsi ya Uingereza) ikawekwa mikononi mwa umma.

Kumbukumbu zinaonesha kuwa April 4, 1974 shirika la umma kusafirisha abiria jijini Dar es Salaam likaanzishwa na kuitwa UDA yaani Usafiri Dar es Salaam. Kadhalika, ikaanzishwa kampuni nyingine kusafirisha abiria kwenda mikoani iliyojulikana kwa jina la KAMATA yaani, Kampuni ya Mabasi Tanzania.

Kutokana na athari zilizotokana na Vita ya Kagera mwaka 1978 hadi 1980, huduma za umma zikaanza kulegalega.
Serikali ikafanya kila linalowezekana kuweka mambo sawa. Katika miaka ya 1980 yakaletwa mabasi aina ya IKARUS kutoka nchini Hungary ili yatoe huduma kusafirisha abiria Dar es Salaam.

Mabasi hayo yalikuwa na muundo kama yalivyo mabasi ya ‘mwendokasi.’ Mabasi marefu yalikuwa na uwezo wa kubeba abiria takribani 150 na mafupi abiria 80; yakaendeshwa na kusimamiwa na UDA. Miaka ilivyoendelea kupita huduma za mabasi ya UDA, ikiwemo ikalusi pia zikaanza kuzorota kutokana na kukosekana vipuli muhimu.

Hali hiyo ikahusishwa na uhaba wa fedha za kigeni, hivyo kushindwa kuagiza vipuli toshelezi pamoja na mabasi kutokaguliwa na kutofanyiwa marekebisho kwa wakati.

Hivyo, Ikalusi yakashindwa kutoa huduma ilivyokusudiwa hadi yakatelekezwa kutokana na shirika kutoendeshwa vizuri ikiwa ni pamoja-na uzembe, kukosa uaminifu na kutowajibika ipazavyo hususani kukosa weledi/utendaji mzuri katika kusimamia shughuli za umma.

Baada ya kuona hali hairidhishi, serikali ikaruhusu sekta binafsi kusafirisha abiria kutoka sehemu mbalimbali hadi katikati ya jiji. Hata hivyo kabla ya hapo, huduma zisizo rasmi zilikuwa zimeanza kutolewa na sekta binafsi kutokana na uhitaji mkubwa wa usafiri kwa kutumia magari yaliyojulikana kama ‘chaimaharage.’

Jijini Dar es Salaam licha ya kuwepo UDA, wakazi kadhaa hutumia usafiri kupitia teksi au yakiwemo magari binafsi.
Kwa wengi, gharama za kukodi magari kila siku ni ‘mtihani mgumu.’ Nakumbuka miaka hiyo nikuwa naishi Mwanayamala ‘A’ na kutokana na adha usafiri, mara kadhaa nilikuwa natembea kutoka katikati ya mji kurudi nyumbani.

Baadaye, serikali ikaruhusu matumizi ya ‘daladala’ na hatimaye ‘bajaji’ na ‘bodaboda’ kurahisisha usafiri wa umma.
Kwa kuzingatia wingi wa watu pamoja-na kuzorota huduma za UDA, serikali iliona ni bora kuanzisha mfumo wa mabasi yaendayo haraka maarufu, mwendokasi.

Kazi ya kujenga barabara mahususi kwa mwendokasi ilianza mwaka 2012 kuanzia Kimara Mwisho hadi Kivukoni; kadhalika, Kimara kwenda Morocco kupitia Magomeni-m Mapipa na Kimara hadi Gerezani (Kariakoo). Huduma za mabasi hayo zikaanza Mei, 2016 chini ya ‘Rapid Transport Dar es Salaam’ (UDA-RT) kupitia barabara zilizotengenezwa kwa ajili hiyo.

Hata hivyo, licha ya juhudi zinazoonekana za serikali kuboresha huduma hizo, tija tarajiwa haijafikiwa maana bado kuna minong’ono ya malalamiko yanayohitaji kuboreshwa zaidi ili kuokoa muda wa Watanzania unaopotea kwa
kusubiri usafiri, badala ya kutumika kuzalisha mali na kukuza uchumi wa watu na nchi kwa ujumla.

Minong’ono mingi ipo kwa abiria wanaotumia njia za kati ya Mbezi-Luis na Kivukoni/ Gerezani na pia, kati ya Kimara- Mwisho na Kivukoni /Gerezani. Dar es Salaam ni ‘BandariSalama’ inatakiwa pia kuwa na usafiri salama, wa uhakika na usiopoteza muda wala kuwapo usumbufu wowote hata wakati wa kukata tiketi.

Kuingia kituoni na kukuta watu wamejazana wakisubiri ‘mabasi’ yanayokawia kisha yakafika yakiwa yamejaza abiria kiasi cha kutosimama kuongeza wengine, ni ‘dhiki juu-ya-dhiki.’

Kwa kuzingatia maboresho yanayoendelea kufanyika kutoka katikati ya jiji kwenda Mbagala- Rangitatu na viunga vyake, Gongolamboto na Tegeta- Bunju pengine hadi Bagamoyo ninashauri mambo kadhaa yaambatane na jitihada hizo.

Hayo ni pamoja na kuwapo mkakati mahususi kuhakikisha yanakuwepo mabasi toshelezi yatakayotoa huduma kwa wakazi Dar es Salaam bila karaha.

Hata hivyo katika hili, napongeza juhudi zinazoendelea kufanyika. Iandaliwe ratiba maalumu inayoonesha basi litafika kituoni muda gani kama ni kila baada ya robo saa au nusu-saa ili anayesafiri azingatie muda kufanikisha lengo lake bila ‘kusota’ kituoni.

Aidha, Watanzania wenye uwezo kiuchumi wahamasishwe kuwekeza kwa kununua mabasi mengi ya ‘mwendokasi’ ili kusaidia kutosheleza mahitaji na kuhudumia abiria kibiashara bila kuwaumiza kwa kutoza nauli kubwa. Jambo hili linahitaji utashi mkubwa wa kisiasa kama ilivyo kwa msukumo sahihi na imara kuhusu nishati safi ya kupikia.

Wahudumu katika vituo vya mwendokasi wawe waadilifu na wanaothamini kazi hiyo kwa kujali usalama na amani kwa abiria wanategemea usafiri huu muhimu kwa maendeleoyao na uchumi wa taifa. Baadhi si waungwana hususani wanaohusika na ukataji wa tiketi kwani lugha zao kunapokuwa na changamoto ya chenji, si nzuri.

Katika vituo vyenye wasafiri wengi, kujengwe miundombinu (maegesho) yatakayowezesha wasafiri wenye magari binafsi kuegesha magari yao na kutumia mwendokasi ili kupunguza msongamano wa magari usio wa lazima katika barabara.

Hili likifanikiwa zaidi, huduma bora na toshelevu za mwendokasi zitakuwa kichocheo kizuri cha watu kufanya kazi kwa muda wote bila hofu ya usafiri na hivyo, kuongeza ufanisi na pia, kuepusha watu kupoteza muda mwingi barabarani kusubiri usafiri, badala ya kuzalisha mali na kutoa huduma.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *