Mwili wa aliyekuwa na deni la Sh milioni 18 wazikwa

BARIADI, Simiyu: Hatimaye mazishi ya marehemu Juma Jumapili (60) ambaye mwili wake ulizuiwa kutolewa kwa siku kadhaa katika Hospitali ya Rufaa Bugando iliyoko jijini Mwanza akidaiwa gharama za matibabu Sh milioni 18 yamefanyika jana katika makaburi ya familia yaliyoko eneo la Sakwe katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu.

Hatua hiyo imekuja mara baada ya kufikiwa kwa muafaka wa deni hilo lililokuwa likidaiwa na Hospitali ya Rufaa ya Bugando iliyoko jijini Mwanza ambapo walibaki na mwili huo tangu Aprili 01 mwaka huu hadi wanafamilia walipotoa malalamiko yao kwa Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Simon Simalenga, wakiomba msaada wa serikali kuwezesha kupatikana kwa mwili huo.

Mkuu huyo wa wilaya alifanya mawasiliano na Hospitali ya Rufaa ya Bugando ambapo mazungumzo yao yalizaa matunda baada ya hospitali hiyo kuruhusu mwili huo uchukuliwe bila familia hiyo kulipa gharama zilizotakiwa.

Simalenga amesema maelekezo ya Rais Samia ni kuwa mwananchi akishindwa kuchukua mwili kwa sababu ya gharama asitozwe bali apewe nafasi ya kuuchukua iwapo suala la malipo limeshindikana.

Imeelezwa kuwa marehemu Jumapili alipata ajali ya pikipiki mwezi Desemba 2023 na alifikishwa kupatiwa Matibabu kwa mara ya kwanza Hospitali ya Wilaya ya Bariadi iliyoko Somanda na baadae kuhamishiwa Hospitali ya Mkoa wa Simiyu iliyoko Nyaumata na pia kupewa Rufaa ya kwenda Hospitali ya Bugando kutokana na hali yake kuzidi kuwa mbaya.

Akizungumza mara baada ya mazishi, Mwali Jumapili ambaye ni ndugu wa marehemu ameelezea hatua walizopitia kupambania kupata msaada wa kulipia gharama za matibabu katika Hospitali ya Bugando hadi umauti ulivyomfika ndugu yao ambapo alieleza walilazimika kuuza Ng’ombe, mashamba na baadhi ya vitu vya thamani ikiwa ni hatua za kugharamia matibabu yake lakini bado walikwama.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button