NALA kuwekeza zaidi ya bil 2/- baada ya kupata ‘baraka’ za BOT

KAMPUNI ya Kitanzania inayotoa huduma ya malipo kwa njia ya kieletroniki, NALA, imepewa leseni na Benki Kuu (BOT) itakayowezesha kufanya biashara hapa nchini.

Baada ya kupata leseni hiyo, NALA inatarajia kuwekeza kiasi cha fedha  kiasi cha dola za Kimarekani milioni moja, sawa na zaidi ya Sh bilioni mbili.

Leseni ya BoT inaifanya NALA kuwa mtoa huduma ya malipo na kuwezesha muunganiko wa moja kwa moja na benki pamoja na waendeshaji wa huduma za kifedha kwa njia ya mitandao ya simu za mkononi.

Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Jumatatu, Afisa Mtendaji Mkuu wa NALA, Benjamin Fernandes amesema uwekezaji huo utaifanya NALA kuboreha huduma na kuongeza wigo wa huduma zake huku wateja wengi zaidi wakinufaika.

Fernandes alisema hatua hiyo itaiwezesha NALA kuanza kutengeneza bidhaa za ziada za kidijitali ambazo zitaongeza ujumuishaji wa malipo, kufanya huduma za malipo ziwe nafuu zaidi na za kuaminika kwa biashara na matumizi ya kawaida.

“Kwa kutumia NALA wateja wanaweza kutuma na kupokea fedha kwa nia ya kijigitali kutoka nchi mbali mbali duniani ikiwa ni pamoja na Marekani, Uingereza, nchi za Jumuiya ya Ulaya na nginginezo,” alifafanua

Mkurugenzi huyo aliafafanua kuwa mara baada ya NALA kuzinduliwa katika Umoja wa Ulaya, kampuni hiyo imepokea leseni yake ya mtoa huduma za malipo nchini Tanzania na kuongeza kuwa hiyo ni hatua kubwa kwa kuwa inatoa nafasi ya kuboresha huduma na kuongeza huduma mpya, kama vile; malipo ya kibiashara, huduma za wafanyabiashara na malipo ya nje kutoka Tanzania, pamoja na ushirikiano wa moja kwa moja na benki za ndani na kampuni za mawasiliano.

“Malengo mawili makubwa ya NALA ya tangu mwaka jana yamekuwa kuwezesha ushirikiano wa moja kwa moja kwa benki na kampuni za mawasiliano ya simu, kukabiliana na changamoto ambazo wafanyabiashara wanazokabiliana nazo katika kuhamisha fedha kuvuka mipaka ya nchi.

“Tumefanya kazi kwa karibu pamoja na Benki Kuu ya Tanzania ili kukamilisha hatua zinazofaa za kupokea leseni yetu kama mtoa huduma wa malipo. Kwa leseni hii mpya mkononi, NALA inapata nafasi na uwezo wa kuendelea na malengo yetu, kubwa likiwa kufanya uwekezaji wenye thamani ya zaidi ya Bilion 2 za Kitanzania ili kujenga miradi yetu mikubwa zaidi kuwahi kutokea katika soko letu la hapa nyumbani Tanzania,” amesema.

NALA ni kampuni ya malipo ya Kiafrika na programu ya kutuma pesa ambayo hukuwezesha kufanya malipo salama na ya kuaminika kutoka Ulaya, Uingereza na Marekani hadi Afrika.

 

Habari Zifananazo

Back to top button