NBS, OCGS zawasilisha ripoti tisa za sensa kwa wadau
MTAKWIMU Mkuu wa Serikali, Dk Amina Msengwa amesema mkakati wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS) ni kuhakikisha taarifa zinazokusanywa zinatumika kwa kuzingatia takwimu rasmi zilizozalishwa.
Dk Mswengwa amesema hayo jijini Dodoma wakati wa kufungua kikao cha kuwasilisha ripoti ambacho NBS na OCGS zimewasilisha kwa wadau ripoti za kina tisa zitokanazo na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
Alisema ofisi hizo zinaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha kuwa taarifa zinazokusanywa hazibaki ndani ya mikono ya NBS na OCGS bali ziwe chachu na mwendelezo wa kuhakikisha kuwa zinaendelea kutumika katika kufanya tathmini bora kwa kuzingatia takwimu rasmi zinazozalishwa.
Awali, Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Makazi na Takwimu za Jamii, Dk Ruth Minja alisema kufanyika kwa kikao hicho ni hatua muhimu ya maandalizi ya ripoti za kitakwimu katika kuhakikisha uchambuzi uliofanyika unakidhi vigezo vya ubora vya ndani na vya Umoja wa Mataifa.
“Hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha ripoti hizo zinaakisi hali halisi ya mahitaji ya takwimu kwa ajili ya kuwezesha kupanga, kupima na kutathmini hali ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya ndani, kikanda na kimataifa,” alisema.
Kwa upande wake, Mtaalamu Mshauri, Dk Dadi Rutasha alisema sensa inaongoza kwa utajiri wa taarifa na kuwa ni chanzo kikubwa cha takwimu kwa ajili ya mipango na sera kwa mamlaka husika na zinaweza kupatikana hadi ngazi ya chini ya jamii.
“Hivyo nihimize matumizi ya taarifa hizi kwa serikali na wadau wa maendeleo katika kuandaa sera mbalimbali,” alieleza.
Ripoti zilizowasilishwa na kuhakikiwa na wadau ni za hali ya makazi na rasilimali za kaya, vifo vya utotoni, vijana wa rika balehe na ujana, ajira na shughuli za kiuchumi pamoja na teknolojia ya habari na mawasiliano.
Ripoti nyingine zilizowasilishwa ni takwimu za mtazamo wa kijinsia, uhamiaji na ukuaji wa miji, vizazi na vifo pamoja na mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar, Salum Kassim Ali alishukuru washiriki na waandaaji wa ripoti hizo na kuwahimiza kufanyia kazi na kukamilisha haraka uboreshaji uliofanywa na wadau ili zizinduliwe na kusambazwa kwa ajili ya kutumika kwenye mipango na sera kwa maendeleo ya jamii.



