NEC yashauriwa kusajili wapiga kura Kidijitali

DAR ES SALAAM: Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeshauriwa mambo manne ikiwemo kutumia mfumo wa kidijitali kusajili wapiga kura wapya kwa kuweka mawakala nchi nzima kama ilivyo mawakala wa kusajili laini za simu.

Hayo yamesemwa leo Septemba 30, 2023 jijini Dar es Salaam katika Mdahalo wa  vijana kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani na uchaguzi mkuu 2025, lililoandaliwa na Asasi ya Kiraia  ya Tanzania Youth Coalition (TYC) kupitia mradi wa  kijana nahodha.

Akiwasilisha mapendekezo ya vijana katika Mdahalo huo, Mwalimu wa masuala ya Demokrasia, Diplomasia na Haki za Vijana, ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Deus Kibamba, amesema mapendekezo manne yaliyotolewa na vijana katika mdahalo huo ni NEC kuanzisha mapema mfumo wa kieletroniki na mawakala kwa ajili ya usajili wa wapiga kura wapya  ili kuwawezesha wananchi kupata haki ya kupiga kura.

“NEC ione umuhimu wa kurahisisha mfumo wa uandikishaji wa kupiga kura wapya, vijana wakitimiza umri wa kupiga kura kuwe na mfumo rafiki wa kujiandikisha kidigitali,  kwa hivi sasa vijana wanangaika kutafuta maisha umwambie akapange foleni kujiandikisha au kupiga kura huwezi kumpata, tumependekeza mifumo miwili.

“Kwanza kujiandikisha mwenyewe, kwa sababu vijana wengi sasa wana simu janja wanaweza kujiandikisha kupitia simu janja, Tume iandae App vijana waweze kujiandikisha, sehemu ya tume iwe kuhakiki taarifa.

“Kuna wengine hawatakuwa vizuri kwenye matumizi ya teknolojia hao nao tumependekeza Tume ya Uchaguzi iende ianzishe mfumo wa mawakala kama ambavyo kuna mifumo ya simu za mkononi kusajili laini kupitia mawakala nchi nzima, hivyo mifumo ya namna hiyo ianzishwe na NEC wa uandikishaji wa wapiga kura wapya.

“Hivi leo kutoka Dar es Salaam mpaka Kigoma mawakala wa kusajili laini za simu wapo, na mfumo unafanya kazi vizuri sana, mfumo huu wa mawakala wa uandikishaji wapiga kura wapya  unafanana sana na huo, yule ambaye hana uwezo wa kusajili mwenyewe, aende kwenye mwavuli wa mawakala ajisajili.”Amesisitiza

Aidha, mapendekezo mengine yaliyotolewa ni umri wa vijana kugombea uwe miaka 18  vyama visiwaminye.

“Kwa sasa vyama vinawaminya sana vijana, badala ya vijana kutumika tu kuhamasisha na kushangilia basi umri wa kugombea uwe  miaka 18 wakati sasa hivi sheria inakataza mtu wa miaka 18 hadi 20 kugombea nafasi yoyote ya uongozi hata ya serikali za mitaa, hivyo imependekezwa marekebisho ya sheria zote bungeni umri huo upitishwe isipokua nafasi ya ugombea Urais.” Amesema Kibamba

Pendekezo la tatu lililotolewa ni eneo la fedha ambalo limependekeza vyama vya siasa visivyo na wawakilishi bungeni, madiwani wala viongozi wa serikali za mitaa kupewa asilimia 20 ya ruzuku ili iwezeshe vijana katika kushiriki michakato ya uchaguzi kwa kuwa vijana wengi hawana fedha za kugharamia michakato hiyo wakati vyama ambavyo wabunge na madiwani wapatiwe ruzuku kwa asilimia 80.

Aidha pendekezo la nne lililotolewa kuanzishwa kwa mfumo wa mgombea huru binafsi kwa kile kilichoelezwa kuwa itasaidia vijana ambao hawana vyama, ambao hawajateuliwa na vyama vyovyote kugombea binafsi.

Habari Zifananazo

Back to top button