NEC yataka ushiriki wa vyama uchaguzi wa kata

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewataka wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wa kata 14 zinazotaraji kufanya uchaguzi mdogo wa udiwani Julai 13, mwaka huu kuvishirikisha vyama vyote vya siasa katika masuala yote ya kiuchaguzi yanayohitaji ushiriki wao.

“Na kama kuna jambo halihitaji ushiriki wao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu, msikubali au msilazimishwe kuvishirikisha vyama hivyo,” alisema Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Thomas Mihayo.

Jaji Mihayo aliyasema hayo mjini Iringa leo wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata.

Advertisement

Baada ya mafunzo hayo alisema Tume inatarajia wasimamizi hao wataifanya kazi ya uchaguzi kwa kuzingatia sheria, kanuni za uchaguzi pamoja na maelekezo ya tume katika utendaji wao.

Jaji Mihayo alisema uchaguzi ni mchakato unaojumuisha, hatua na taratibu mbalimbali za kufuatwa ili kuufanya uwe mzuri, wenye ufanisi na hivyo kupunguza au kuondoa kabisa malalamiko au vurugu wakati wote.

“Katika mafunzo haya msione haya kuuliza jambo lolote msilolielewa ili msije mkaenda kuuendesha uchaguzi huu kwa mfumo wa mazoea,” alisema.

Kuhusu wasimamizi wa vituo vya kupigia kura, Jaji Mihayo; “Mkaajiri watendaji wa vituo wenye weledi, wanaojitambua na kwa kadri inavyowezekana kuacha undugu au upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawana sifa za kufanya shughuli za uchaguzi.”

Aidha amewata wasimamizi hao kuhakikisha wanayatambua na kuyajua vizuri maeneo ambayo chaguzi utaendeshwa ikiwemo hali ya miundombinu ya kufika katika kata na vituo vya kupigia kura.

“Mfanye utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema ili kubaini mahitaji maalum ya vituo husika kwa lengo la kuhakikisha mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani,”alisema.

Awali Mkurugenzi wa NEC, Ramadhani Kailima alizitaja kata zitakazofanya uchaguzi huo hkuwa ni Ngoywa iliyopo halmashauri ya wilaya ya Sikonge na Kalola-Uyui zote za mkoani Tabora.

Zingine ni Kata ya Sindeni-Handeni, Potwe-Muheza, Kwashemshi-Korogwe, na Bosha-Mkinga zote za Mkoani Tanga.

Kwa mujibu wa bosi huyo wa NEC, kata zingine ni Mahege ya Kibiti Pwani, Bunamhala- Bariadi mkoani Simiyu, na Njoro na Kalemawe za Same mkoani Kilimanjaro.

Aidha, uchaguzi huo mdogo utazihusu kata ya Mnavira katika halmashauri ya wilaya ya Masasi mkoani Mtwara na Kinyika-Njombe, Magubike-Kilosa mkoani Morogoro na Kata ya Mbede- Mpimbwe mkoani Katavi.

Mkurugenzi huyo amesema ratiba ya uchaguzi huo itaanza na utoaji wa fomu za uchaguzi kwa wagombea kuanzia Juni 24 hadi 30, 2023 huku uteuzi wa wagombea watakao wania nafasi hizo ukitarajiwa kufanyika Juni 30 mwaka huu.

Mapema kabla ya ufunguzi wa Mafunzo hayo watendaji wa uchaguzi hao walikula kiapo cha kutunza siri na kiapo cha kujitoa uanachama wa vyama vyao vya siasa.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *