Ni hatari kuzidisha vijiko 5 vya asali, sukari
JAMII imehimizwa kutumia asali au sukari vijiko visivyozidi vitano kwa siku ili kuepukana na uwezekano wa kupata magonjwa ya kisukari.
Mwenyekiti wa Chama cha Kisukari Tanzania-TDA-Profesa Andrew Swai ametoa onyo hilo Dar es Salaam leo katika semina ya viongozi mbalimbali wa dini.
Prof Swai ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Magonjwa yasiyo ya kuambukiza Tanzania amesema asali haina tofauti na sukari vyote ni sawa kwani ikiingia mwilini haraka inaweza kuleta matatizo.
SOMA: Ongezeko ugonjwa wa kisukari, watakiwa kuzingatia haya
“Ukitumia asali tayari imejaa sukari kwa kuwa ni majimaji huna njia ya kuzuia ikae nje, itaingia mwilini haraka na itakuletea matatizo, ndio sababu tunawaambia watu wasitumie sukari au asali ikizidi inachoma ndani,”amesema.
Pia, amesema vyakula vyote vya wanga vina sukari inayoingia mwilini polepole kwa sababu mpaka chakula kisagwe iende kwenye utumbo mdogo ibadilishwe na kugeuka kuwa sukari na hivyo, kuhimiza kupunguza utumiaji wa vyakula hivyo.
Amesema sukari ikizidi nguvu mwili huunguza mishipa ya fahamu, moyo na matokeo yake husababisha wengi wenye kisukari kupata magonjwa ya macho, figo, mishipa ya fahamu na mengine.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa magonjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Omary Ubuguyu amesema kuwa viongozi wa dini wana nafasi kubwa zaidi ya kukutana na wanajamii na kuwapa elimu juu ya uwepo wa magonjwa yasiyoambukiza na kuwapatia ushauri wa kujijengea utamaduni wa kupenda kujua hali za afya zao kupitia kwa wataalam wa afya.
Mtaalam wa lishe kutoka Taasisi ya Lishe Tanzania Adeline Munuo amesema viongozi wa dini watumie fursa ya kuwashawishi waumini wao kushiriki kuzuia magonjwa yasiyoambukizwa kwa kuhimiza watu kwenda hospitali kupima na kujua afya zao ili kupata matibabu mapema.