KATI ya mambo ya hatari yanayoweza kusababisha mtu apoteze maisha ni pale anapokosa msaada wa huduma ya kwanza anapokabiliwa na ugonjwa au madhara ya ghafla wakati daktari hayupo karibu na kabla hajapelekwa hospitalini kwa matibabu zaidi.
Hali hiyo huweza kumtokea mtu yeyote kulingana na mazingira na aina ya ugonjwa wenyewe uliomkumbuka na endapo hatopata msaada wa haraka huweza kupata athari kubwa au kupoteza maisha.
Ni wazi kuwa suala la huduma ya kwanza limekuwa likizungumzwa mara kadhaa na watalaamu wa afya, serikali na wanaharakati lakini kiukweli bado halijapewa uzito wake katika maeneo mengi nchini.
Hivi karibuni, katika eneo lenye mkusanyiko wa watu kutokana na shughuli za maziko, kulitokea tatizo la watu kadhaa kupoteza fahamu kutokana na mshituko lakini cha ajabu, umati mkubwa uliokuwepo eneo hilo ulionekana wazi kutokuwa na ufahamu wa namna ya kuhudumia mtu aliyepatwa na mshtuko.
Wengi wa watu hao walijikusanya na kuwazingira wale waliopoteza fahamu, huku kila mmoja akitamka njia ya kumsaidia nyingi zikiegemea zaidi katika imani na si kitaalamu jambo lililozidi kuwatia hatarini wahusika.
Endapo kusingekuwa na watu wawili katika msiba huo wenye utalaamu wa masuala ya afya akiwemo mmoja aliyekuwa muuguzi mstaafu ni wazi kuwa, watu wale waliopoteza fahamu kutokana na mshtuko na wengine ama presha kupanda au kushuka wangeweza hata kupoteza maisha.
Wataalamu hao wawili walifanyakazi kubwa ya kuwaondoa watu waliowazunguka wagonjwa huku wakipiga kelele za kutaka wapatiwe hewa lakini pia walazwe kwa kichwa kuwa chini na miguu juu ili waweze kupata hewa.
Pamoja na hayo, ilibidi wafanye kazi ya ziada ya kuwaelekeza watu kadhaa kuwalaza kichalichali wagonjwa hao wa ghafla juu ya sehemu iliyo ngumu, isiwe kitandani, kuwapunguzia nguo zilizopo kifuani, kubinua kichwa kidogo, kubonyeza kwa nguvu kifua kwa wastani wa dakika moja pamoja na kumuwahisha mgonjwa hospitali.
Ukweli ni kwamba, katika tukio hilo ilionyesha wazi ni jinsi gani jamii haina ufahamu wa namna ya kutoa huduma ya kwanza kwa watu wanaougua ghafla kabla ya kukimbizwa hospitali.
Jamii inapaswa kupewa mafunzo na kutambua kuwa huduma ya kwanza husaidia kuokoa maisha, kupunguza maumivu na kuzuia hali ya mgonjwa isizidi kuwa mbaya lakini pia husaidia kuharakisha uponaji kabla ya mgonjwa kupata matibabu hospitalini.
Ifike mahala mamlaka husika zione umuhimu wa kuanzisha progamu maalumu za kijamii kwa ajili ya kuelezea namna ya watu kusaidiana wanapokutwa na magonjwa yanayohitaji mtu kupatiwa huduma ya kwanza.
Yapo matukio mengi yanayoweza kufanywa kwa njia ya huduma ya kwanza kabla ya mgonjwa hajafikishwa hospitali na kumsaidia kama vile, mtu kuzama kwenye maji, kukatwa na chupa, kung’atwa na wadudu wenye sumu kama vile nyoka au nge, kuungua, kunywa sumu, kupanda au kushuka kwa presha na ajali.
Matukio yote hayo yanatakiwa jamii husika kuwa na elimu ya kutosha juu ya jinsi ya kuyakabili kabla ya mgonjwa kufikishwa hospitalini la sivyo badala ya kusaidia watazidi kumuumiza mgonjwa husika au pengine hata kumdhuru.
Hiyo ni kutokana na ukweli kuwa magonjwa mengine kama ajali, kung’atwa na mdudu mwenye sumu, kuungua au kunywa sumu endapo mgonjwa asipopewa huduma ya kwanza hasa kama huduma za afya ziko mbali, afya na maisha yake yanaweza kuwa hatarini.
Hivyo basi, mamlaka husika zinazoshughulikia masuala ya afya wadau mbalimbali na asasi za kijamii zinazowajibu wa kuhakikisha zinatumia mbinu mbalimbali za kuwafikishia mafunzo sahihi wananchi juu ya namna ya kutoa huduma ya kwanza kwa wagonjwa.