DAR-ES-SALAAM: MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imewataka wananchi ambao vitambulisho vyao vimepata hitilafu ya kufutika maandishi wavirejeshe katika ofi si zake. Pia wananchi wanaweza kuvipeleka katika ofisi za serikali za mitaa, kata, vijiji na shehia ambako vitakusanywa na kurejeshwa kwa ajili ya kuchapishwa upya bila malipo yoyote kwa mwananchi.
Mkurugenzi wa Idara ya Vitambulisho Nida, Edson Guyai alisema Dar es Salaam kuwa wamepokea taarifa kuwa kuna vitambulisho vichache vimefutika taarifa zalizochapwa mbele au nyuma ya kitambulisho.
SOMA: Vitambulisho vya Nida vitolewe mapema waishio mipakani
Guyai aliwaeleza waandishi wa habari kuwa takwimu za Nida zinaonesha kuwa vitambulisho vyenye hitilafu hiyo ni 21,224 sawa na asilimia 0.09 ya vitambulisho 21,32,098 vilivyozalishwa. Alisema serikali iliwezesha Nida Sh bilioni 42.5 kwa ajili ya ununuzi wa kadi ghafi na baada ya kuwezeshwa taasisi hiyo ilipanga na kutekeleza mkakati wa uzalishaji na usambazaji wa vitambulisho.
Guyai alisema: “Nida imezalisha vitambulisho takribani vya watu wote waliokuwa NIN kwa muda mrefu na kuvipeleka huko kwenye ofisi nilizozitaja”.
Amesema kuna vitambulisho vingi havijachukuliwa na kwamba wananchi waende wakachukue vitambulisho vyao.
Hatahivyo amesema kumekuwa na upotoshaji kuhusu ubora wa vitambulisho vya taifa kutokana na changamoto hiyo iliyojitokeza.
SOMA: https://nida.go.tz/swahili/
Alisema vitambulisho vinavyotolewa na mamlaka hiyo vina ubora unaokidhi viwango vya kimataifa. Guyai alisema hitilafu ndogo ni jambo la kawaida kutokea katika sekta ya uzalishaji wa bidhaa duniani.
Aliwataka watendaji wa serikali za kata, mitaa, vijiji, vitongoji Tanzania Bara na shehia kwa upande wa Zanzibar wavikusanye na kuvirejesha kwenye ofisi za Nida wilayani vichapishwe upya bila malipo yoyote kwa mwananchi. Kuhusu kasi ya uchukuaji wa vitambulisho vya taifa, Guyai alisema si ya kuridhisha hasa katika maeneo ya mijini kwa kuwa kuna takribani vitambulisho milioni mbili ambavyo havijachukuliwa na wahusika.