Norway yaisifu Tanzania jitihada kukabili mabadiliko ya tabianchi

SERIKALI ya Tanzania imeishukuru Serikali ya Norway na Shirika la Maendeleo la Norway (NORAD) kwa mchango wake katika kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya Tanzania.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni alisema hayo katika makao makuu ya Norad jijini Oslo Norway alipokutana na kuzungumza na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Bard Vegar Solhjell.

Mazungumzo baina ya viongozi hao yalilenga kujenga na kuimarisha uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Norway kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabianchi, mazingira pamoja na tafiti zinazofanyika kwa ufadhili wa Norad.

“Tanzania inathamini sana mchango mkubwa unaotolewa na Norad katika masuala ya kiufundi, kifedha, utunzaji wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, uhifadhi wa misitu na utekelezaji wa mradi wa REDD,”alisema Masauni.

Alisema shirika hilo limechangia kwa kiasi kikubwa katika upatikanaji wa nishati mbadala na usambazaji wa umeme vijijini.

“Ushirikiano wa Norad umekuwa muhimu katika kuendeleza maisha ya jamii, ufahamu wa mazingira, na uwezo wa kitaasisi,” alisema Masauni.

Solhjell aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada za kukabili mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na kuanzisha Kituo Cha Taifa Cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC).

Kupitia mazungumzo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Maendeleo Endelevu katika Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Norwary, Marita Sorheim Rensvik, ujumbe wa Tanzania kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais ulipata fursa ya kusikiliza mawasilisho ya miradi ya mazingira inayotekelezwa na Serikali ya Norway katika maeneo mbalimbali duniani ikiwa ni pamoja na nchini Tanzania.

Serikali ya Norway imekuwa ikitekeleza miradi nchini ikiwa ni pamoja na masuala ya kilimo, elimu, utafiti, hali ya hewa na mazingira.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button