UJUMBE wa watu kutoka Serikali ya Norway umetembelea ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma kuona maendeleo ya mpango wa kunusuru kaya maskini.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa na nchi za Nordic, Anne Beathe Tvinnereim aliongoza ujumbe huo.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alisema Anne ameambatana na Balozi wa Norway nchini, Elizabeth Jacobsen na Balozi wa Tanzania nchini Norway, Grace Olotu.
Norway ni nchi ambayo inasaidia Tanzania kupambana na umaskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambao kwa sasa upo katika awamu ya tatu ya utekelezaji wake ambao ulianza mwaka jana.
“Niushukuru ujumbe huu kwani Tanzania ina mikoa 26 lakini wao wamependelea kutembelea makao makuu ya nchini mkoani Dodoma. Wakiwa Dodoma ujumbe utatembelea Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kuwakilisha wilaya zingine za Mkoa wa Dodoma ili kujionea hali halisi ya utekelezaji wa miradi ya Tasaf mkoani Dodoma,” alisema na kuongeza:
“Pamoja na kusaidia kuondokana na umaskini nchini, Tasaf inajihusisha na masuala ya mazingira na hasa mabadiliko ya tabianchi.”
Serikali ya Norway imeahidi kuongeza fedha zitakazotumika katika masuala ya tabianchi. Pia imeahidi ushirikiano katika masuala ya kilimo ambayo yanagusa kundi kubwa la Watanzania.
Senyamule aliueleza ujumbe huo kuwa asilimia 80 ya Watanzania ni wakulima na asilimia 72 ya watu wa Dodoma wanajishughulisha na kilimo. Alisema msaada katika sekta ya kilimo utasaidia katika kupunguza umaskini kwa kiasi kikubwa.
Alikaribisha wafanyabiashara wa Norway kuwekeza Dodoma. Aliuambia ujumbe huo kuwa pamoja na uwekezaji, Tanzania imebarikiwa kwa maeneo mengi yenye vivutio vingi vya utalii kama vile Serengeti, Ngorongoro, Manyara hivyo ni mahali salama na pazuri kwa utalii.
Mratibu wa Tasaf Mkoa wa Dodoma, Bogit Semhanda alisema kipindi cha kuanzia Januari 2021 hadi Juni 2022, Mkoa wa Dodoma umepokea Sh 11,409.402,636 kutoka Tasaf na kusambazwa kwenye halmashauri nane.
Kati ya kiasi hicho, Sh 10,040,274,319 zimetumika kulipa wanufaika 71,669 kati ya 80,317 kutoka katika vijiji 564 na mitaa 231.
Katika kipindi cha Mei hadi Juni, 2022, Mkoa wa Dodoma umepokea Sh 3,067,680,484 zilizotolewa na uongozi wa Tasaf kwa ajili ya malipo kwa wajane. Mpaka sasa Sh 596,601,000 zimelipwa kwa kaya 13,977 ambazo ni sawa na asilimia 19 ya wanufaika.