MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) imetumia Sh bilioni 2.6 kuwalipa watumishi 183 waliofutiwa ajira kwa kukutwa na vyeti feki.
Haya yameelezwa jijini hapa na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba wakati wa kueleza utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mfuko na mwelekeo wa watendaji katika mwaka wa fedha 2022/23.
Alisema katika nusu ya mwaka wa fedha iliyoishia Desemba 2022, Mfuko ulilipa mafao ya Sh bilioni 350.7 kwa wanachama, wastaafu na wanufaika wengine wapatao 80,339.
“Malipo haya yanajumuisha Sh bilioni 2.6 zilizolipwa kwa watumishi 183 waliofutiwa ajira kwa kukosa vyeti halali.”
Hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan aliridhia watumishi walioondolewa kazini kutokana na vyeti feki kulipwa fedha za michango waliyochangia katika kipindi cha ajira zao kwa fedha zilizokatwa kwenye mishahara yao pekee.
Akifafanua zaidi, Mshomba alisema NSSF bado inaendelea kuwalipa watumishi wao lakini hatarajii idadi kuongezeka zaidi kutokana na mfuko huo kuwa na idadi ndogo ya watumishi wa umma waliokuwa wakichangia mfuko huo.
Mshomba alisema katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 2023, Mfuko unatarajia kulipa mafao yenye thamani ya Sh bilioni 769.3 ambayo ni ongezeko la asilimia 17 ukilinganisha na Sh bilioni 659.8 zilizolipwa katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2022.
“Katika eneo hili la mafao, napenda kumshukuru tena Rais Samia kwa kuridhia ombi la vyama vya wafanyakazi la kuja na kikokotoo kipya kwa ajili ya manufaa ya wastaafu wetu ambacho kilianza kutumika Julai 2022.”
Kutokana na mabadiliko ya kikokotoo, sasa wastaafu wanapokea mkupuo wa awali wa asilimia 33 ukilinganisha na asilimia 25 ambayo wastaafu wa NSSF walikuwa wanapata.
“Jambo la muhimu hapa ni kwamba kikokotoo hiki kinazingatia uendelevu wa mifuko yetu ya hifadhi ya jamii.”
Aidha, Mshomba alisema katika nusu ya mwaka wa fedha iliyoishia Desemba 2022, Mfuko ulikusanya michango ya Sh bilioni 807.6 sawa na asilimia 1 juu ya lengo la makusanyo ya kipindi hicho.
Alisema katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 2023, Mfuko unatarajia kukusanya michango ya Sh trilioni 1.6 ambayo ni ongezeko la asilimia 14 ukilinganisha na michango ya Sh trilioni 1.4 iliyokusanywa na Mfuko katika mwaka wa fedha ulioishia mwezi Juni 2022.
Mshomba alisema pia Mfuko uliandikisha wanachama wapya 123,340 na idadi ya wanachama wachangiaji katika Mfuko ilifikia wanachama 1,109,997.
Alisema pia katika nusu mwaka, Mfuko ulikusanya Sh bilioni 165.7 kutokana na mapato ya uwekezaji na vitega uchumi vya Mfuko.
Katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 2023, thamani ya vitega uchumi vya Mfuko inatarajiwa kukua na kufikia Sh trilioni 6.3 ambalo ni ongezeko la asilimia 17 kutoka Sh trilioni 5.4.