Nyusi wa Msumbiji kuanza ziara Tanzania

DAR ES SALAAM – RAIS wa Jamhuri ya Msumbiji, Filipe Nyusi (65) anawasili nchini leo kwa ziara rasmi ya kitaifa na kikazi ya kuimarisha uhusiano na biashara.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba alisema pia kiongozi huyo anakuja kuwaaga Watanzania akijiandaa kumaliza muhula wa pili wa kuiongoza nchi hiyo.

January aliwaeleza waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa ziara hiyo ya siku nne inafanyika kwa mwaliko wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Alisema Rais Nyusi anawasili nchini leo katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA). January alisema kiongozi huyo atafanya ziara ya kitaifa kuanzia Julai Mosi hadi pili mwaka huu na kwamba baada ya kuwasili leo atapokelewa na viongozi wa serikali na kesho atapokelewa Ikulu, Dar es Salaam na mwenyeji wake Rais Samia.

Alisema baada ya kufanya mazungumzo ya faragha viongozi hao watafanya pia mazungumzo rasmi na kisha watazungumza na waandishi wa habari na kisha watashuhudia kusainiwa mikataba kwenye maeneo matatu.

January aliyataja maeneo hayo kuwa ni afya, mashirika ya habari na elimu na kuongeza kuwa lengo la ziara ya Rais Nyusi pamoja na mambo mengine ni kuimarisha uhusiano na ushirikiano kwenye masuala ya biashara.

“Biashara baina yetu sio nzuri sana, tunataka tuimarishe ili tufanye zaidi biashara, ukiangalia kwa takwimu za mwaka jana, tulifanya biashara na Msumbiji ya Dola za Marekani milioni takribani 17 wakati mwaka uliotangulia tuliuza zaidi ya Dola za Marekani milioni 57, tunataka tuimarishe eneo hilo,”alisema January.

SOMA: Waziri Mkuu apongeza uongozi mpya TEC

Aidha alisema Tanzania na Msumbiji watu wake wanafanya zaidi biashara maeneo ya mpakani ambayo taarifa zake hazirekodiwi hivyo kuchangia kuonesha kiwango cha biashara ni kidogo.

Kuhusu kuimarisha usalama kwenye mpaka wa Tanzania na Msumbiji, January alisema hali ni nzuri na Tanzania na Msumbiji wana ushirikiano katika masuala ya usalama na ulinzi na kuwa askari wa Tanzania kupitia mwavuli wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wako Msumbiji kuimarisha usalama.

Alisema askari wengine wapo nchini Msumbiji kupitia mahusiano ya nchi mbili ambayo yamo chini ya Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ulinzi na Usalama ya Tanzania na Msumbiji na kuwa wameendelea kuimarisha usalama baada ya hali ya usalama kuzorota nchini humo, hususan kwenye Jimbo la Cabo Delgado.

“Ziara hii itasaidia kudumisha na kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na marais wawili watafanya majadiliano kwenye nyanja mbalimbali, elimu, usalama, miundombinu, madini mafuta na gesi na nchi zote nimegundua kiwango kikubwa cha gesi bahari kuu,”alisema January.

Akizungumzia eneo la pili la ziara hiyo, January alisema Rais Nyusi anafanya ziara ya kikazi nchini na Julai 3 mwaka huu atafungua Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) katika Viwanja vya Sabasaba.

 

View this post on Instagram

 

A post shared by HABARILEO (@habarileo_tz)

Alisema baada ya kufungua maonesho hayo Rais Nyusi ataenda Zanzibar kwa ziara binafsi na kisha atarejea Msumbiji Julai 4, mwaka huu kupitia Kiwanja Cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Aman Karume.

January alisema Rais Nyusi pia anakuja kuwaaga Watanzania na Rais Samia baada ya kumaliza muhula wake wa pili wa uongozi wake akiwa rais wa taifa hilo ambalo linakwenda kufanya uchaguzi mkuu Oktoba, mwaka huu kuwapata viongozi wapya.

Rais Nyusi aliingia madarakani Januari 15, mwaka 2015 akiwa rais wa nne wa taifa hilo lililopata uhuru mwaka 1975. Ziara ya mwisho ya Rais Nyusi nchini ilikuwa Januari 11, 2021, alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja kwa kuweka jiwe la msingi, ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanza-Chato mkoani Geita.

Katika ziara hiyo, Rais Nyusi alipokelewa na mwenyeji wake Rais wa awamu ya tano John Magufuli.

Habari Zifananazo

Back to top button