ACT Wazalendo kuongeza thamani ya bidhaa

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT–Wazalendo, Othman Masoud Othman, amesema serikali atakayoiongoza itaweka mkazo katika kuzipa thamani bidhaa zinazozalishwa visiwani humo ili ziweze kutambulika na kushindana katika masoko ya kimataifa.
Akizungumza na wajasiriamali na wauzaji wa samani katika eneo la Mkokotoni, Othman alisema Zanzibar imekuwa na historia ndefu ya ubunifu katika kazi za mikono na useremala, lakini changamoto za masoko na mifumo mibovu ya kiuchumi zimezorotesha maendeleo ya sekta hiyo.

“Serikali ya ACT–Wazalendo itahakikisha wajasiriamali wadogo wanapatiwa mikopo nafuu, elimu ya biashara na mafunzo ya kisasa ili bidhaa zao ziweze kufikia viwango vya kimataifa,” alisema Othman. SOMA: Hemed aahidi kufufua michezo Kiwani
Aliongeza kuwa serikali yake itaweka utaratibu wa masoko ya kimataifa kwa bidhaa za asili za Zanzibar kama samani, vinyago, bidhaa za mwani, viungo na nguo zenye muundo wa Kizanzibari, hatua itakayosaidia kuinua uchumi wa wananchi.
Othman alisema Zanzibar ina utajiri mkubwa wa ubunifu na bidhaa zenye ubora wa kipekee ambazo zinaweza kutoa ajira kwa vijana na wanawake endapo zitatunzwa na kuendelezwa kwa sera madhubuti. Alitoa wito kwa wananchi wa Zanzibar kufanya maamuzi ya mabadiliko kwa kumchagua kiongozi mwenye dhamira ya kuendeleza rasilimali zao na kuziweka katika mfumo wa kisasa unaonufaisha wote.


