Elimu ya faragha yafikishwa kwa wasioona

TUME ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imeanza mkakati maalum wa kuwafikia watu wenye mahitaji maalum kwa kuwapa elimu ya faragha na kuelimisha kuhusu haki zao wanapokuwa kwenye mitandao ya kijamii.
Akizungumza wakati wa mafunzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam kwa ajili ya Jumuiya ya Watu Wasioona Tanzania (TAB), Mwanasheria kutoka PDPC, Humprey Mtui amesema tume itaendelea kutoa mafunzo kwa kila kundi nchini ili wananchi waweze kulinda taarifa zao binafsi na kufahamu haki zao. “Tume itaendelea kutoa elimu ya taarifa binafsi kwa makundi yote. Hii itatusaidia kufikisha malengo ya tume ya kulinda haki na faragha za wananchi,” alisema Mtui.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watu Wasioona (TAB), Omary Itambo amesema mafunzo hayo yatawasaidia wanajumuiya hiyo kulinda taarifa zao binafsi. “Watu wengi wa kundi hili wamekuwa wakisahaulika, hasa katika masuala ya kidigitali. Tumefarijika sana kuona tume imetukumbuka kutupa mafunzo haya,” alisema Itambo.
Hatahivyo, Itambo ameishauri PDPC ifikie pia mikoa ya pembezoni kama Katavi, Kigoma, Rukwa na Mbeya ili wanajumuiya hao pia waweze kupata mafunzo ya ulinzi wa taarifa na kufahamu haki zao. SOMA: Sheria kulinda faragha za watu yaanza kutumika
PDPC imeendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya jamii ikiwemo wafanyabiashara, watumiaji wa huduma za kidijitali, na washiriki wa matukio ya kitaifa, huku ikiendeleza jitihada za kuongeza uelewa wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na namna ya kulinda haki za faragha.



